Rais mstaafu wa awamu ya nne ambae pia ni mkulima wa matunda ya mananasi,Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wamiliki wa viwanda vya matunda kuacha kuwakandamiza wakulima kwa kununua matunda kwa gharama ya chini.
Amesema viwanda hivyo vinasaidia kupatikana kwa masoko ya ndani lakini vimekuwa havina uwiano wa gharama zinazolingana na maumivu anayoyapata mkulima.
Aidha Dkt. Kikwete ameeleza kumekuwa na changamoto ya kushuka kwa soko kwa wakati mwingine hali inayokuwa ikisababisha wakulima kupata hasara kwa matunda kuoza yakiwa mashambani.
Hayo ameeleza wakati akitoa taarifa ya shamba lake la mananasi lililipo Bago-Kiwangwa Wilayani Bagamoyo, wakati Mwenge wa Uhuru ulipokwenda kutembelea shamba hilo.
Rais mstaafu Dkt. Kikwete alieleza, viwanda vya usindikaji matunda mbalimbali vinapaswa kumjali mkulima ambae amekuwa akipata shida na kutumia gharama kubwa kuandaa shamba.
“Wakati utafika watakosa matunda, kutokana na gharama yao hailipi, wakulima wa matunda tushindwa kukubali kuuza kwa bei ya chini ambayo hailipi ” .
Hata hivyo Rais huyo mstaafu alimwambia kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa 2017, Amor Hamad Amor, kuwa mananasi huvunwa baada ya miezi 18 tangu kupandwa.
“Bei ya mauzo hutegemea wanunuzi na wachuuzi wadogowadogo ambao hununua kwa ukubwa wa nanasi sh 400 hadi 800 linapovunwa kutoka shambani.
Dkt. Kikwete alisema, shamba lake lina ukubwa wa hekari 200 ambapo hekari 64 ndizo zimelimwa na zipo kwenye hatua ya palizi.
“Mwenge kwa kuangaza shambani kwangu ni ishara ya nuru, basi nitapata neema baadae, nashukuru kwa kuja kutembelea shamba langu kujionea shughuli ninazofanya baada ya kustaafu” alisema Rais mtaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Kiongozi huyo pia alipita kujionea shughuli za ujenzi wa kiwanda cha Sayona kinachomilikiwa na kampuni mama ya MMI Steel, kilichopo kata ya Mboga.
Afisa Uhusiano wa Kampuni za MMI Steel ikiwemo Sayona, Abubakar Mlawa, alimwambia kwamba, kiwanda cha Sayona kimefikia asilimia 70 ya ujenzi na mwezi Novemba mwaka huu kinatarajia kuanza kazi.
Alieleza kuwa kiwanda hicho, kwasasa kimeajiri watu 100 wakiwemo mafundi ujenzi na kitakapoanza kazi kitaajiri watu 800.
Mlawa alisema, mahitaji makubwa ni matunda zaidi ya tani tisa kwa siku, hasa maembe, nyanya na matunda mengine hivyo wakulima wa matunda wachangamkie fursa hiyo.
Alisema kiwanda cha Sayona ni moja ya uwekezaji mkubwa Mkoani Pwani, na kinalenga kugharimu dola milioni 55 sawa na shilingi bilioni 120 katika ujenzi wake.
Nae kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Amor Hamad, alipongeza Serikali kwa kuondoa ushuru wa mazao ya matunda na kuongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi hali inayoonyesha taifa kutaka kukuza soko la ndani.
Alimpongeza Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Kikwete na kuwataka wakulima wa zao hilo kuiga mfano wake wa kulima kwa tija .
Amor aliwataka wananchi kujishughulisha kwa kufuata nyayo za waasisi wetu akiwemo Kikwete na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda .
“Niipongeze Serikali kwa jitihada hizo kwani inaonyesha Serikali inataka kukuza soko la ndani ya nchi na wakulima kuthaminika ili kujiletea maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.