Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Peter Billa, leo amepokea ugeni kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA Taifa, Mhandisi Ruth S. Koya, kwa ziara ya siku mbili yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maji na utendaji wa vyombo vya kijamii vya huduma ya maji vijijini (CBWSOs).
Katika kikao kifupi kilichofanyika ofisini kwa Katibu Tawala, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Beatrice Kasimbazi, alieleza kuwa ziara hiyo itafanyika katika Halmashauri za Wilaya ya Kibaha na Bagamoyo, na itaambatana na ukaguzi wa miradi ya maji pamoja na kikao cha tathmini kuhusu changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake, Mhandisi Koya alisema ziara hiyo inalenga pia kupata tathmini ya moja kwa moja kutoka kwa wananchi kupitia vyombo vya usimamizi wa huduma za maji, pamoja na kufanya ufuatiliaji wa utendaji wa RUWASA katika ngazi ya mkoa.
“Kutembelea miradi pamoja na kukutana na vyombo vya usimamizi wa huduma za maji kutatuwezesha kupata taarifa ya moja kwa moja kutoka kwa wananchi kuhusu hali ya huduma hizi,” alisema Mhandisi Koya.
Akitoa neno la shukrani, Kaimu Katibu Tawala. Peter Billa aliwapongeza viongozi hao kwa juhudi wanazofanya katika kusimamia huduma ya maji vijijini na kusisitiza kuwa ziara za namna hiyo ni muhimu kwani zinatoa picha halisi ya changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maji.na kuahidi ushirikiano wa karibu na RUWASA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.