Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Mhandisi Kundo A. Mathew, amepongeza uongozi wa Mkoa wa Pwani chini ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, kwa utekelezaji wa vitendo wa sera za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta ya maji. Jitihada hizi zimepelekea ongezeko la upatikanaji wa maji mkoani Pwani, ambalo sasa limefikia asilimia 86.
Mheshimiwa Kundo alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, ambapo alifanya kikao kazi na wataalamu wa sekta ya maji na kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya maji. Ziara hiyo imelenga kuimarisha juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
Katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma kwa wananchi na aligiza kuanzishwa kwa kitengo maalum cha kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya maji. Aidha, alielezea mafanikio ya miradi ya majisafi na usafi wa mazingira inayotekelezwa na serikali kwa manufaa ya wananchi.
“Tupo hapa kuhakikisha maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanatekelezwa kwa vitendo. Ni haki ya kila mwananchi kupata maji safi na salama, lakini pia taarifa sahihi kuhusu huduma za maji endapo kutakuwa na changamoto,” alisema Mheshimiwa Kundo.
Mheshimiwa Kundo alibainisha kuwa awali upatikanaji wa maji mkoani Pwani ulikuwa asilimia 59, lakini juhudi za serikali ya awamu ya sita zimefanikisha ongezeko hilo kufikia asilimia 86. Pia alipongeza juhudi za wadau wa maji, hususan DAWASA, kwa kubuni miradi mikubwa kama ule wa Rufiji unaotarajiwa kuzalisha maji mara tatu zaidi ya sasa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, alimshukuru Naibu Waziri kwa ziara yake, akisema kuwa itachochea maendeleo ya sekta ya maji na kufanikisha dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.
“Mkoa wetu unakua kwa kasi kutokana na uwepo wa viwanda na ongezeko la makazi. Tunahitaji huduma bora ya maji, na ujio wa Mheshimiwa Naibu Waziri unaleta matumaini makubwa kwa wakazi wa Pwani,” alisema Mheshimiwa Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.