Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Eng. Kundo A. Mathew, ameipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa juhudi zake za kusimamia miradi ya maji vijijini. Alieleza kuwa juhudi hizo zimepunguza changamoto ya upatikanaji wa maji, ikiunga mkono azma ya Serikali ya kumtua ndoo mama kichwani.
Mheshimiwa Kundo alisema hayo alipotembelea na kukagua Bwawa la uzalishaji maji katika Kitongoji cha Mjembe, Kata ya Kibindu, Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani. Mradi huo wenye gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja, uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya watu 3,000 wa kijiji hicho.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Kundo alitoa agizo kwa RUWASA kuhakikisha mtandao wa maji kutoka Bwawa la Mjembe unakamilika ifikapo tarehe 30 ya mwezi huu.
Aidha, aliwataka kufanya usanifu wa haraka kwa vijiji vyote vya Kata ya Kibindu ili maji yaweze kusambazwa katika maeneo yote ya kata hiyo. “Nawaagiza RUWASA kuhakikisha mtandao wa maji kutoka Bwawa la Mjembe unakamilika ifikapo tarehe 30 mwezi huu. Hakikisheni pia mnafanya usanifu wa haraka ili maji yawafikie wananchi wote wa Kata ya Kibindu,” alisema Mheshimiwa Kundo.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Eng. Beatrice Kasimbazi, alieleza kuwa kazi ya usambazaji maji katika kijiji cha Mjembe imeanza, huku vifaa vyote muhimu vikiwa tayari.
Aliongeza kuwa mradi huo uko katika hatua za mwisho za utekelezaji, na wananchi wa kijiji hicho wanatarajiwa kuanza kunufaika na maji safi na salama mara baada ya mtandao wa maji kukamilika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.