Halmashauri zote Mkoani Pwani zimetakiwa kuhakikisha kuwa zinajibu hoja zote kwa wakati na kuhakikisha kuwa zinafungwa kwa wakati
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikillo, wakati wa kikao maalum cha baraza la madiwani cha kujadili hoja za mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG Wilayani Rufiji.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa maelekezo ya Serikali ni pamoja na kuzitaka halmasahuri zote kuzijibu hoja kwa wakati na kuhakikisha kuwa hoja hizo zinafungwa.
Aidha amezipongeza halmasahuri zote za Mkoa Pwani kwa namna walivyofanya kazi ya kusimamia matumizi mazuri ya fedha za Serikali kitu kilichoziwezesha kupata hati safi.
Alisema kuwa kupata hati safi sio kazi ndogo kwani inahitaji kufanyakazi vizuri pamoja na kuheshimu fedha za serikali, amewataka wasibweteke bali waendelee kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia taratibu kwani kwa mwaka anataka kuona hati safi tena.
Pia amezitaka Halmashauri hizo kuainisha vyanzo vyote halisi vya mapato na kusisitiza kuwa visimamiwe ili viweze kukusanya mapato vizuri
Mhandisi Ndikilo alisisitiza kuwa hatokuwa tayari kumfumbia macho mtendaji yeyote Yule ambaye atafanya uzembe na kuisababishia Hasara Halmashauri.
Pia aliwataka wakurugenzi waiimarishe kitengo cha ukaguzi katika Halmashauri zao na kuwataka wakaguzi wote wa ndani kuwa makini katika kufanyakazi za kuzisimamia Halmashauri kutumia vyema fedha za serikali na amewataka kufanyakazi kwa weledi pasipo kumuogopa mtu.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ndikilo ameipongeza Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa Pwani kwa namna walivyofanya ukaguzi kwa kufuata sheria na taratibu za ukaguzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.