Timu ya soka ya Mgomba ya wilayani Rufiji imetwaa ubingwa wa Siro Super Cup 2018 kwa kuifunga Mjawa ya wilaya ya Kibiti kwa penati 11-10.
Mchezo huo ulichezwa mwishoni mwa wiki hii katika uwanja wa Samora uliopo Wilayani Kibiti ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo.
Timu hizo hadi zinamaliza muda wa kawaida wa dakika 90 zilishindwa kufungana na kufanya matokeo kuwa 0-0 ndipo zikaingia hatua ya penati ambapo Mgomba walipata penati zote 11 na Mjawa waliokuwa wenyeji wakipata penati 10 na kukosa moja.
Kutokana na ushindi huo Mgomba walifanikiwa kujinyakulia kiasi cha fedha taslim shilingi 1,000,000/=,kombe,seti ya jezi na medali ya dhahabu huku Mjawa wakijinyakulia kiasi cha shilingi 500,000/= seti ya jezi na medali fedha na mshindi wa tatu timu ya Mipeko kutoka wilaya ya Mkuranga wakijinyakulia 300,000/=.
Mfungaji bora Dickson Mhilu alijinyakulia mpira huku mwamuzi bora akijinyakulia jezi kwenye mashindano hayo yaliyokuwa na kauli mbiu ya Kibiti salama Jamii salama.
Akifungua Mashindano hayo ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amepongeza kiwango kizuri kilichoonyeshwa na timu zote mbili katika mchezo huo na ametoa rai kwa wadau wa soka kufika vijijini kuvumbua vipaji vya wanamichezo badala ya kuangalia mijini pekee.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amewaasa wakazi wa Kibiti na Rufiji kudumisha amani iliyopo kwa sasa kwani pasingekuwa na amani kwenye maeneo hayo basi hata michezo hiyo isingeweza kufanyika .
“Mnapofurahia kushiriki katika michezo hii mkumbuke kuwa furaha yetu itaendelea kudumu kama mtatambua kuwa usalama ndio unaotufanya tuwepo hapa,bila usalama ndugu zangu tusingeweza kuwa hapa leo tungekuwa kila mmoja amekaa kwenye eneo lake kwa kuhofia usalama .
Adui yetu mkubwa ni uhalifu wa aina yoyote, ni matumaini yangu kuwa hivi sasa kila mmoja wetu anaelewa vya kutosha juu ya madhara ya uhalifu, ni wajibu wangu kama kiongozi na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kuwakumbusha juu ya hatari inayoweza kuwakuta tena endapo hamtachukua hatua madhubuti za kuzuia na kutokomeza aina zote za uhalifu.Nawaasa kila mmoja katika nafasi yake kushiriki katika shughuli za ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya ulinzi na usalama”alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa mashindano hayo yamedumisha upendo na kuondoa tofauti baina ya wakaazi wa Wilaya tatu za Kibiti,Mkuranga na Rufiji kwa kushiriki katika mashindano hayo kwa mshikamano wa hali ya juu.
Mashindano hayo ambayo yalianza mwezi Aprili yaliandaliwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenerali (IGP) Simon Siro na kushirikisha kata 54 za wilaya hizo za kanda Maalumu ya Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.