.Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amewaapisha wakuu wa Wilaya wapya Mhe. Jokate Mwegelo wa wilaya ya kisarawe na Mhe. Zainab Kawawa wa Wilaya ya Bagamoyo na kutoa maagizo 16 ya kutekelezwa na wakuu wa wilaya hizo.
Moja ya maagizo hayo ni pamoja kuhakikisha kila mkuu wa wilaya anasimamia ukusanyaji wa mapato na kufikia asilimia zaidi ya 25 ifikapo septemba mwaka huu pamoja na kuhakikisha wamiliki wa makampuni wanapatiwa namba za utambulisho ( TIN) za biashara zao ndani ya mkoa badala ya kukatiwa Dar es Salaam kama baadhi yao wanavyofanya na kuunyima mkoa mapato.
Hafla ya kuwaapisha wakuu hao wa wilaya ilifanyika kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa vilivyopo wilayani Kibaha.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa, wakuu wa wilaya wanapaswa kufanyia kazi suala la makusanyo ya mapato kuhakikisha kuwa mapato ya halmashauri yanakuwa si chini ya asilimia 25 .
Aidha aliwataka wakuu hao wa wilaya,kuhakikisha wanadhibiti na kusimamia vyanzo vya mapato ya ndani ikiwemo mchanga na kokoto ili kujua vinaingiza mapato kwa kiasi gani .
“Kuhusu taarifa ya mkaguzi mkuu wa serikali CAG alisema halmashauri zote za mkoa zimepata hati safi lakini msibweteke simamieni sekta zote ili tuendelee kupata hati safi wakati wote.
Pia alimtaka Mkuu mpya wa wilaya ya Bagamoyo ,kudhibiti magendo kwenye bandari bubu zaidi ya 19 zilizopo Bagamoyo ambazo zinainyima serikali mapato.
Aidha aliwataka waheshimiwa Jokate Mwegelo na Zainab Kawawa kwenda kuuliza kwenye wilaya zao kama kuna kamati za amani na kama hazipo hakuna waunde kamati hizo mara moja.
“Hakikisheni mnadhibiti migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji kwani kwa mkoa wa Pwani damu iliwahi kumwagika kwenye wilaya za Bagamoyo, Kisarawe, Rufiji na Chalinze alisema mhandisi Ndikilo “
Alisisitiza utunzaji wa hifadhi za misitu na kuilinda ili isivamiwe na kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kukata mkaa,kuni na mbao .Katika hilo ,alimuasa Mhe. Jokate na Mhe. Zainabu kwenda kusimamia hifadhi ya misitu mikubwa ya Kazimzumbwi -Kisarawe na Uzigua na Ruvu Kusini na Kaskazini-Bagamoyo.
“Nasisitiza maelewano baina ya viongozi wa ngazi mbalimbali kwani baadhi yao hawaelewani hili ni tatizo ambalo halipaswi kuendelea kwani wanaoumia ni wananchi ambao wanapaswa kuongozwa,” alisema Ndikilo.
Kuhusu sekta ya maji ,alimuagiza mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mhe Jokate kumsimamia mkandarasi wa maji kutoka Mloganzila kwenda Kisarawe ili akamilishe kazi kwa wakati alisema tatizo la maji ni kubwa wilayani humo hivyo ahakikishe anakuwa mstari wa mbele kushirikiana na mkoa kuusukuma mradi huo ukamilike ili kumtua ndoo mama kichwani.
Kwa upande wao wakuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe ,Jokate Mwegelo na Zainab Kawawa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo walisema wamepokea maagizo yote na watayafanyia kazi.
Mhe.Jokate alieleza ,hatomuangusha Mhe.Rais, Mkuu wa Mkoa na wananchi wa Kisarawe na kudai hajaenda kutengua torati bali anakwenda kuiimarisha,na kuwaomba wananchi na watendaji wa wilaya yake wote wakutane kazini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.