Serikali Mkoani Pwani imewaagiza maafisa tarafa wote kutimiza majukumu yao bila uzembe na badala yake wahakikishe wanashughulikia migogoro ya ardhi ambayo inawakabili kwa kiasi kikubwa jamii ya wafugaji na wakulima kwani inapelekea kuwepo kwa uvunjifu wa amani na baadhi ya wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa halfa ya kukabidhi Pikipiki 28 zenye thamani ya shilingi 148,176,000.00 ambapo Pikipiki 27 zimekabidhiwa kwa Maafisa Tarafa wa tarafa zote za mkoa pwani na Pikipiki moja imebaki kwa ajili ya Matumizi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha Ndikilo amewataka maafisa hao tarafa kuweka mikakati madhubuti katika utekelezaji wa majukumu yao hususan katika ufuatiliaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuwaletea maendeleo chanya wananchi.
“Katika Mkoa wa Pwani katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi kwa hivyo ili suala inatakiwa maafisa tarafa kuifuatilia wenyewe na kuimalizi sio mpaka viongozi wa ngazi za juu waende kuitafutia ufumbuzi hivo ninawaomba katika hili tujitahidi kwa hali na mali ili kuondokana na hali hii ikiwemo suala la mimba kwa wanafunzi na utoro yote myafanyie kazi,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Theresia Mmbando amebainisha kuwa hapo awali maafisa tarafa walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na usafiri wa uhakika hivyo kushindwa kutimiza majukumu yao kwa wakati katika kuwaatumikia wananchi katika suala zima la kuleta maendeleo.
Nao baadhi ya maafisa tarafa ambao wamenufaika na kupatiwa Pikipiki hizo wamesema kwamba zitaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufiuatilia na kusuluhisha kwa urahisi changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi kwani hapo awali walikuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na usafiri wa uhakika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.