MKuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Evarist Ndikilo amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani kuhakikisha kwamba wanaihudumia timu ya Mkoa wa Pwani ambayo imeteuliwa kwenda kushiriki mashindano ya UMISETA Kitaifa Mkoani Mwanza.
Hayo ameyasema mwanzoni mwa wiki hii wakati akifunga mashindano ya UMISETA Kimkoa ambayo yalifanyika katika viwanja vya Filbert Bayi ambapo wanafunzi 120 walichaguliwa kuunda timu ya Mkoa.
Mhandisi Ndikilo aliziagiza pia Halmashauri hizo kuwa na sare ambayo itaitambulisha Halmashauri husika ambapo amesema kwa mwaka ujao hataki kuona wanamichezo wakiwa hawako katika sare.
“Ni lazima kila Halamashauri ziwe na trakisuti nzuri kwa ajili ya wanamichezo na si kama walivyo sasa ambapo kila mmoja amejivalia tu” alisema Ndikillo
Aidha, ameagiza pia kila shule lazima iwe na kiwanja cha michezo na kutaka vipindi vya michezo mashuleni virudishwe. Mhe. Ndikilo amesema kuwa kila shule ikiwa na kiwanja cha michezo itawasaidia vijana kupata fursa ya kufanya michezo kwani michezo ni ajira.
Katika hatua nyingine Mhe. Ndikilo amewataka Wanamichezo hao kwenda kuuwakilisha Mkoa wa Pwani vizuri katika michezo hiyo na kuweza kurudi na ushindi pamoja medali nyingi.
“Napenda kuchukua fursa hii sasa kuwapongeza wote mlioteuliwa kuwakilisha Mkoa wetu, tunawataka sasa mkawe Mabalozi wazuri wa Mkoa wa Pwani, Mkapeperushe bendera ya Pwani muende mkapambane ili muweze kuleta medali, Mkoa wa Pwani umewatuma na mkajitume ili mlete Medali “alisema Ndikilo.
Aidha Mhandisi Ndikilo pia aliwataka wachezaji hao wawe na mshikamano na wawe na nidhamu ya hali ya juu ambayo itawasaidia katika kupata ushindi.
Timu hiyo ya Mkoa itashirikisha michezo ya Mpira wa Miguu wavulana na wasichana, Mpira wa wavu Wavulana na wasichana, Mpira wa Mikono wavulana na wasichana, Mpira wa Pete wasichana, Mpira wa meza Wavulana, Riadha wavulana na wasichana na mchezo wa sanaa ngoma, kwaya, Ngonjera na Mashairi.
Mashindano hayo ya UMISETA yalianza tarehe Mei 26, 2018 na kumalizika Mei 28,2018 ambapo yalishirikisha Halmashuri zote tisa za Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.