Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wananchi waliovamia eneo la Pangani Wilayani Kibaha lenye ukubwa wa hekari 500 na kujigawia viwanja kuondoka mara moja,ili kuiacha Halmashauri kufanya taratibu ya kurudisha eneo hilo Serikali, baada ya mmiliki wake kushindwa kuliendeleza na kuwa sehemu ambayo watu wanauawa na kutupwa humo.
Aidha amelitaka jeshi la polisi kumkamata mtu yoyote atakayekutwa kwenye eneo hilo, na kuwataka wale wahusika ambao ni matapeli waweze kukamatwa kwa kuwauzia watu kinyume cha sheria kwani eneo hilo linamilikiwa kihalali.
Mhandisi Ndikilo aliyasema hayo alipotembelea eneo hilo ambalo linamilikiwa na mtu anayefahamika kwa jina la seamens na maeneo mengine yenye ukubwa wa hekari 500 yanayomilikiwa na watu wengine wawili ambao hawajaendeleza kwa muda mrefu, hivyo wananchi kujigawia viwanja wakidai kuwa eneo hilo limekuwa sehemu ya wahalifu kufanya mauaji, au kutupa maiti kutoka maeneo mbalimbali.
Alisema kuwa kuna watu 18 ambao wanajifanya ndiyo viongozi na wamewagwia watu hatua 30 kwa 30 kwa kila mtu katika eneo hilo ambalo wahalifu wamelifanya eneo hilo kwa ajili ya kupumzika baada ya kufanya uhalifu au wanapowateka watu au kuwaua.
“Kuanzia sasa sitaki kuona mtu katika eneo hili na jeshi la polisi naligiza likamate mtu yoyote watakayemkuta humu, na achukuliwe hatua kwani ardhi haipatikani kwa njia hizo, kwa sasa acheni Serikali iendelee na taratibu zake za mchakato wa kurudisha eneo hili na mengine ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu, kwani kwa sasa mamlaka zinazohusika zinaendelea na urejeshwaji eneo hilo serikalini, kwani liko chini ya mmiliki wake hadi hati ya eneo hilo itakapofutwa”alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa kwa wale waliouziwa watoe taarifa polisi, ili wahusika waliouza Ardhi wakamatwe, na Mkuu wa Wilaya awasake watu hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao, kwakua hawawezi kuuza eneo la mtu ambaye anamiliki kisheria hata kama hajaendeleza kwani kuna taratibu zake za kumiliki ardhi lakini si kwa njia hiyo.
“Tunajua kuna mahitaji makubwa ya ardhi lakini si kwa utaratibu huu mchakato unaendelea tutapeleka mapendekezo kwa Waziri wa ardhi nyumba na makazi naye atapeleka kwa Rais kwa ajili ya kufuta umiliki, kisha Halmashauri litapanga utaratibu na kuwagawia wananchi kutegemea na mahitaji ya viwanja na mipango miji. mmiliki hatarudishiwa kwani alisema kuwa anataka kukata viwanja ili auze hapana”alisema Ndikilo.
Aliitaka hiyo kamati iliyounda na kuwazuia watu warudishe fedha kwa wale waliowauzia kwani wamewatapeli na Serikali haiwezi kulifumbia macho jambo hilo kwani mara baada ya kurudi litapangiwa utaratibu kwani kwa sasa mji huo unapangwa ili kuelekea kuwa manispaa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa wananchi hao kutoka maeneo mbalimbali ya Kibaha na Dar es Salaam waligawana maeneo hayo ambayo yanamilikiwa na watu watatu.
Mshama alisema kuwa mmiliki wa kwanza eneo lake lina ukubwa wa hekari 300,mwingine hekari 200 na mwingine hekari 500. ambapo wananchi waliamua kugawana viwanja kinyume cha sheria wakidai kuwa eneo hilo limekuwa likitumika kwa vitendo vya kihalifu.
“Walisema wameamua kugawana eneo hilo wakidai kuwa wamiliki wameshindwa kuendeleza na kufanya baadhi ya watu wakiuwawa humo hasa waendesha pikipiki au maiti kutupwa kwenye eneo hilo ambalo halijaendelezwa na kuwa msitu”alisema Mshama.
Alisema kuwa baada ya kutokea uvamizi huo wamiliki walifika Ofisi ya Mkurugenzi na kutakiwa kujieleza ni kwa nini wameshindwa kuyaendeleza na kuwataka watoe mpango wa maeneo yao ambapo wengine walitaka kukata viwanja na kuviuza jambo ambalo walikataliwa kwani wameshindwa kuyaendeleza kwa muda mrefu hivyo mchakato wa kuyarudisha Serikalini umeanza.
Naye mmbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini silvestry Koka alisema kuwa eneo hilo lina wamiliki hivyo ni vema kukaa nao na kuona watawekaje mipango miji ikoje ya Serikali katika kuupanga mji wa Kibaha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.