Waziri wa nchi, OR-TAMISEMI Ummy Mwalimu ameelekeza ofisi yake kugharamia ujenzi wa shule mbili za Sekondari kwenye Kata ya Kawawa na Gwata halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ili kuwaondolea adha ya ukosefu wa shule na kuwawezesha wanafunzi katika maeneo hayo kuendelea na masomo.
Waziri Ummy alitoa maelekezo hayo baada ya kukagua madarasa Sita na ofisi tatu katika shule mpya ya Sekondari Disunyara-Mlandizi iliyojengwa na halmashauri hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 120 na kuwezesha kupunguza mlundikano wa wanafunzi katika shule ya sekondari Kilangalanga iliyokuwa na zaidi ya wanafunzi 2100.
“TAMISEMI Itajenga shule ya Sekondari Gwata na leo ninaongeza shule nyingine ya Sekondari ninayoelekeza ijengwe Mtongani na ujenzi wa madarasa na maabara kwenye shule hizi uanze mara moja.” Alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy alifikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Nuru Butamo Ndarahwa iliyosema kuwa halmashauri hiyo inazo Kata 14 lakini kuna shule za Sekondari kwenye Kata saba tu.
Waziri Ummy pia ameahidi kuhakikisha kuwa shule ya Sekondari Disunyara inakamilishiwa usajili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.