Serikali ya Mkoa wa Pwani imesema itaendelea kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi waliostaafu na waliopoteza maisha wakiwa kazini kadri ya makusanyo ya mapato ya ndani yatakavyopatikana.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge leo Juni 22, 2023 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha maalum kilichoketi kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG.
Amesema anatambua uwepo wa madai ya watu katika Halmashauri za mkoa huo na kwamba hatua mbalimbali zimeendelea ili kuhakikisha wastaafu wote wanalipwa stahiki zao.
Amefafanua kuwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, tayari wastaafu wameanza kulipwa kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato kikiwemo cha fedha zitokanazo na mauzo ya viwanja ambapo kilitolewa kiasi ili kulisaidia kundi hilo.
“Natambua kuna wastaafu wanazidai halmashauri zetu, hatuwezi kumaliza kwa wakati mmoja madeni haya lakini tunachokifanya ni kutumia vyanzo vyetu vya mapato ya ndani kupunguza madeni haya, niwaombe watumishi muendelee kuwa wabunifu na kuanzisha vyanzo vingine vya mapato ili kushughulikia vikwazo kama hivi,” amesema Kunenge.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Butamo Ndalahwa, aliliambia baraza la madiwani kuwa suala la madai ya watumishi wastaafu limekuwa likiwaumiza kichwa na kwamba wanaendelea kupambana kuhakikisha wanalipa stahiki za watu hao.
Ameongeza kuwa madai hayo yamedumu kwa muda mrefu hali inayosababisha kila mwaka kwenye ripoti ya - CAG kuingia kwenye hoja hivyo wanatamani kukamilisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.