Mkoa wa Pwani unajipanga kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara na uwekezaji nchini kupitia maonesho makubwa ya biashara na uwekezaji yatakayofanyika Disemba 16 hadi 20, 2024, katika viwanja vya Mailimoja, Kibaha Mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari Disemba 2, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alisisitiza umuhimu wa maonesho hayo katika kukuza uchumi wa mkoa na kufungua milango ya fursa kwa wafanyabiashara, wawekezaji, na wajasiriamali. Kunenge alieleza kuwa maonesho haya ni mwendelezo wa jitihada zilizofanikiwa katika awamu za miaka ya 2018, 2019, na 2022.
Kunenge alibainisha kuwa lengo kuu la maonesho haya ni kutangaza fursa za uwekezaji, kufungua masoko mapya, na kutoa jukwaa la kuonyesha bidhaa zinazozalishwa mkoani Pwani. Maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha washiriki 550, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wa kati, na taasisi za umma na binafsi.
“Maonesho haya ni nafasi adimu kwa kila mshiriki kujifunza, kushirikiana, na kupata fursa mpya za uwekezaji. Wananchi wanakaribishwa kwa wingi kutembelea maonesho haya na kujionea ubunifu wa bidhaa na huduma zinazotolewa mkoani Pwani,” alisema Kunenge.
Katika hatua nyingine kunenge akieleza kuwa maonesho haya yataambatanan na kongamano la uwekezaji ilitakalofanyika Disemba 18 ambalo litafanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha kwa Mfipa. Kongamano hilo litahudhuriwa na washiriki 400, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za serikali na sekta binafsi, na litatoa nafasi ya mijadala juu ya maendeleo ya biashara na uwekezaji.
Kunenge alitaja pia mafanikio makubwa ya Mkoa wa Pwani chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa mkoa huo umeongeza viwanda 78 vikubwa tangu 2021, na kufikia jumla ya viwanda 1,553. “Tunaendelea kunufaika na mazingira bora ya uwekezaji yaliyoimarishwa na serikali. Maonesho haya ni sehemu ya juhudi zetu za kutekeleza dira ya maendeleo ya viwanda nchini,” aliongeza Kunenge.
Pia ametoa wito kwa wadau wa sekta mbalimbali kushiriki katika maonesho haya ili kujifunza, kupata ushauri wa kitaalamu, na kuonyesha bidhaa zao. “Hii ni fursa ya kipekee kwa wafanyabiashara na wawekezaji kukuza mitandao ya kibiashara, kuboresha maarifa, na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla,” alisema.
Maonesho haya yanatarajiwa kuwa kielelezo cha mabadiliko chanya kwa uchumi wa Mkoa wa Pwani, huku yakiimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kukuza uwekezaji na biashara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.