Mkoa wa Pwani umejipanga kuimarisha mapambano dhidi ya malaria kwa kusambaza vyandarua milioni 1.2 vyenye thamani ya shilingi bilioni 24.
Hatua hiyo inalenga kufikia kaya 454,593 zenye zaidi ya wananchi milioni 2.2 katika wilaya saba na halmashauri tisa za mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akizungumza Septemba 9, 2025 wakati wa uzinduzi wa usambazaji na ugawaji wa vyandarua hivyo, alisema shughuli hiyo inatekelezwa na Bohari ya Dawa (MSD) kwa mwongozo wa serikali.
"Lengo kuu ni kulinda afya za wananchi hususan watoto, wajawazito na familia kwa ujumla," alisema huku akihimiza wananchi kutumia vyandarua kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuvigeuza kwa matumizi mengine.
Aliongeza kuwa kila kaya inapaswa pia kuchukua tahadhari zingine ikiwa ni pakoja na kuondoa mazalia ya mbu na kutumia dawa za kunyunyizia, ambazo kwa sasa huzalishwa katika kiwanda kilichopo Mjini Kibaha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Victor Sungusia, alisema Mkoa wa Pwani ni wa tatu kunufaika na mpango huo kitaifa baada ya Shinyanga na Kigoma na akabainisha kuwa magari 30 yametengwa kwa ajili ya zoezi hilo na watatumia siku 21 kukamilisha usambazaji na kuwa MSD imekwishasambaza zaidi ya vyandarua milioni 40 tangu kuanza kwa mpango huo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, alifafanua kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu, timu za afya zilitembelea kata 111 na vijiji 553 na kubaini kaya 454,593 sawa na asilimia 110 ya lengo zitakazopokea vyandarua hivyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.