Kampeni ya Samia Legal Aid, inayolenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, inazinduliwa rasmi mkoani Pwani tarehe 24 Februari 2025 katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Mailimoja, Kibaha.
Kampeni hii, inayodhaminiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila kikwazo cha gharama.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, amesema kampeni hii ni hatua muhimu kwa wananchi, hasa wale wenye changamoto za kisheria katika masuala ya ndoa, mirathi, ardhi, na mengineyo.
“Kampeni hii siyo tu kwamba inaleta msaada wa kisheria, bali pia inahamasisha wananchi kuelewa haki zao. Ni fursa kwa wote wenye malalamiko kufika na kusikilizwa,” alisema Kunenge.
Kwa mujibu wa Kunenge, kampeni hiyo itaendelea kwa siku tisa, kuanzia tarehe 25 Februari hadi 5 Machi 2025, ikiwapa wananchi muda wa kuwasilisha matatizo yao na kupata suluhisho la kisheria.
Tayari, kampeni hii imeshatekelezwa katika mikoa 19 ya Tanzania, na Pwani inakuwa mkoa wa 20 kunufaika na huduma hii muhimu. Wananchi wa mkoa huo wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hii ya kipekee ya msaada wa kisheria bila gharama yoyote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.