Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewapongeza wakulima wa Zao la Pamba wa Halmashauri ya Chalinze kwa kulima zao la pamba kwa wingi ambapo zao hilo linaonyesha kustawi sana Mkoani Pwani.
Pongezi hizo amezitoa alipofanya Ziara yake ya kuhamasisha kilimo cha pamba katikaHalmashauri ya Chalinze na kuvitembelea Vijiji vya kata ya Mbwewe,Mandera na Miono, ambapo Mhandisi Ndikilo aliweza kuona shamba la mfano la zao la Pamba katika Kijiji cha Kwamkonje na kuona jinsi zao hili inavyostawi katika Halmashauri ya Chalinze.
Katika kuhamasisha zao hilo Mhandisi Ndikilo amewataka Wananchi wa Chalinze na Mkoa Pwani kwa ujumla kupambana na hali ya umaskini kwa kulima mazao ya biashara ikiwemo Pamba na Korosho kwani mazao haya yanastawi vizuri katika Mkoa wa Pwani.
“Napenda kutoa rai kwa wananchi wa mkoa Pwani hasa wananchi wa Chalinze na Rufiji tumieni fursa hii ya kulima Pamba kwani Mkoa wetu una ardhi nzuri yenye rutuba inayafaa kwa kilimo cha pamba na korosho ,kwani mazao haya ni mazao ya biashara ambayo yatatusaidia kuondokana na umaskini”alisema Ndikilo.
Katika Hatua nyingine Ndikilo aliwataka wakulima wa zao la Pamba kuzingatia masharti na kanuni za kilimo bora katika uzalishaji ili kujenga thamani na kutoliharibu zao la pamba kwa kuchanganya na mchanga au maji kwani kufanya hivyo hupelekea kuua soko la zao hilo .
“Napenda kuwaasa wananchi kuwa tuache kuhujumu zao la pamba kwani tutajiharibia soko na tutakuta tunarudi kule kwenye umaskini ,hivyo yeyote atakaebainika kuwa anahujumu zao la Pamba basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”alisema Ndikilo
Aidha Ndikilo alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze kwa kuweka mipango ya kununua pikipiki kwa ajili ya Maafisa Ugani na kuwataka maafisa hao kuweza kuwafikia wakulima na kuwasaidia kutumia mbinu bora za kilimo ili kuliongeza thamani zao la Pamba.
“Nimefarijika na taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze lakini pia kauli ya Mwenyekiti wa Halmashauri kwamba zao la Pamba linakubalika na pia nimejionea mwenyewe” Mhandisi Ndikilo alisema.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliweza pia kukagua kiwanda cha kuchambulia pamba kilichopo Kijiji cha Mandera ambacho kwa sasa hakifanyi kazi, na aliahidi kuwa atafanya kila awezalo ili aweze kufufua kiwanda hicho.
Mhandisi Ndikilo pia alitembelea msitu wa Uzigua kwa lengo la kuona maendeleo ya msitu huo ambapo alishuhudia uoto wa asili umeanza kurudi, na hali ya msitu imeanza kurejea katika hali yake, na wanyama wameanza kuonekana ingawa alielezwa kuwa bado ipo changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo yao kinyemelea. Ndikilo aliagiza kuwa, zoezi la kuwaondoa wafugaji liwe endelevu kwa maslahi mapana ya msitu huo, ambao ni mapito ya wanyama wanaotoka Mbuga ya Sadan kwenda Wamimbiki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.