Mkoa wa Pwani umeanza kutangaza azma mpya ya Utalii wa Mafia kwa kuanzisha maonesho ya Wiki ya Utalii katika Wilaya ya Mafia.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema Maonesho hayo yatafanyika katika Visiwa hivyo mapema Mwaka huu kwa kuwashirikisha wadau wa Utalii kutoka ndani na nje ya Visiwa hivyo.
Amesema lengo la maonesho haya ni kutangaza na kukuza sekta ya utalii ili iweze kukuza uchumi wa kisiwa cha Mafia na Tanzania kwa ujumla.
Amewataka wadau wa utalii pamoja na wananchi wa Visiwa vya Mafia kwa ujumla wao kujiandaa na maonesho hayo ili yaweze kufanyika kwa ufanisi na kuleta tija iliyokusudiwa.
Akiongea katika kikao na wadau wa utalii Wilayani Mafia Mhe.Ndikilo amesema kuwa wiki hiyo itakuwa ni ya kimkoa ambapo Wilaya zote za Mkoa Pwani zenye vivutio vya utalii zitashiriki katika maonesho hayo.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwaambia wadau wa utali kwamba tumenuia kuinua Sekta ya utalii katika Visiwa vya Mafia.”alisema Mh.Ndikilo
Amewahakikishia wadau wa utalii kwamba hali ya kisiwa cha Mafia ni salama na hakuna maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19.
“Nimetoka katika kituo chetu cha Afya cha Kirongwe ambacho kilikuwa kikitumika kama kituo cha matibabu ya wagonjwa wenye COVID 19 ambacho kilikuwa na wagonjwa watano na Wagonjwa wote walitibiwa wakapona na mpaka sasa nimejiridhisha hakuna mgonjwa hata mmoja” alisema RC Ndikilo.
Sambamba na hilo ameeleza kuwa usafiri wa Mafia kwa sasa umeimarishwa kwani ujenzi wa Meli ya Serikali umefika hatua nzuri na inatarajia kuanza safari zake mwezi Julai mwaka huu ,pia tunayo Meli ya Mtu binafsi inayoitw MV Captain one ambayo yatari inafanya safari zake kati ya Mafia -Nyamisati.
“Mafia sasa inafunguka rasmi kwani ile ahadi ya Mh. Rais Dkt John Pombe Magufuli imekamilika na tutaizindua Meli hiyo ya Serikali mwezi Julai na kuanza kazi, sasa tutaona ni jinsi gani maendeleo yatakayofanyika kisiwani hapa na tunataka kuiona Mafia Mpya” alisema Mhe.Ndikilo
RC Ndikilo amesema kuwepo kwa Meli hizo mbili sasa itapelekea Kufunguka kwa Milango ya Mafia katika masuala ya kiuchumi na Kitalii pamoja na kuiongezea Halmashauri Mapato ya ndani.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wadau wa sekta ya utalii katika Visiwa vya Mafia wameomba kuboreshewa mazingira katika fukwe za Utende pamoja kupunguzwa kwa tozo inayotozwa na Hifadhi ya Bahari (Marine Park) ya dola 25 kwa kila mtalii anayeingia katika maeneo ya hifadhi hiyo.
Akiwa Wilayani Mafia Mhe. Ndikilo aliweza kutembelea miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa wilayani humo na alipata nafsi ya kuongea ma wananchi wa Kijiji cha Chole.
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.