Mkoa wa Pwani umeweka rekodi ya kipekee kwa kujipanga kutekeleza zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo ndani ya kipindi kifupi cha siku 30 pekee, tofauti na muda wa miezi miwili uliopangwa kitaifa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaib Ndemanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani katika ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, katika kijiji cha Miono, Wilaya ya Chalinze. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo.
“Tunajua nyie kama Wizara mmepanga kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi hili kwa miezi miwili, lakini nikuhakikishie Mhe. Waziri, Mkoa wa Pwani kwa furaha tuliyonayo na namna tulivyopokea zoezi hili, tutahakikisha tunamaliza ndani ya siku 30,” alisema Mhe. Ndemanga kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amepongeza uongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani kwa kujitokeza kwa wingi na kupokea kampeni hiyo kwa uzito unaostahili, akisema ni sehemu ya kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha sekta ya mifugo.
“Tunaendelea na majadiliano na nchi tano ambazo zinaonesha nia ya kuchukua mifugo yetu ikiwa hai. Hii inadhihirisha kuwa soko la mifugo lipo, na hapa Pwani tuna kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama ambacho sasa kinaweza kufikia uwezo wake wa asilimia 100, tofauti na sasa ambapo kinafanya kazi kwa asilimia 50,” alifafanua Mhe. Dkt. Kijaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Bw. Ngobere Msamau, ameishukuru serikali kwa kuwaletea chanjo hizo, huku akiahidi kuwa wafugaji wataendelea kufuata maelekezo na ushauri wa serikali kutokana na manufaa wanayoanza kuyaona.
Ziara ya Mhe. Dkt. Kijaji ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, iliyoanzishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 16 Juni 2025 katika Wilaya ya Bariadi, mkoa wa Simiyu. Kampeni hiyo inaendelea katika mikoa mingine, ikiwemo Morogoro ambapo Waziri atazuru tarehe 10 Julai 2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.