Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria katika Mkoani Pwani, vimepungua kutoka 124 kwa mwaka 2016 na kufikia vifo 57 sawa na asilimia 9.6 mwaka 2017.
Pamoja na hilo ,kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2015 -2017 wagonjwa wa malaria walioripotiwa katika zahanati ,vituo vya afya na hospitali Mkoani humo ,walikuwa 720,181.
Hayo yalibainika katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo , na waandishi wa habari na kuelezea kuwa Mkoa umeandaaa kampeni ya uhamasishaji wa kununua na kutumia dawa ya kuulia viluwiluwi vya mbu waenezao ugonjwa wa Malaria, ambazo zinazalishwa katika kiwanda cha Tanzania Biotech Product Ltd kilichopo Kibaha.
Mhe. Ndikilo alieleza kuwa ,kutokana na takwimu hizo ugonjwa huo bado ni hatari hivyo Mkoa umejipanga kuhamasisha na kuongeza matumizi ya dawa ya viuadudu ili kudhibiti mbu waenezao malaria.
“Kwa kuzingatia kwamba kiwanda cha dawa hizi kipo hapa kwetu na kuwa maambukizi ya malaria kimkoa bado yapo juu takriban asilimia 15 zaidi ya maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia 14, tumedhamiria kuongeza matumizi ya dawa hiyo”
“Kwa uzoefu kwa wenzetu nchini Cuba ambao walianza kutumia viuadudu vya kuua mbu wa malaria kabla yetu wamefanikiwa kutokomeza kabisa ugonjwa huo ” alisema Mhandisi Ndikilo.
Pia alisema kuwa ,katika uhamasishaji huo Mkoa unakusudia kufanya mambo mawili ikiwemo kuufahamisha umma kuwa dawa ya kutokomeza malaria ipo Kibaha kwa kutoa elimu kwa vitendo ya matumizi na kuzigawa dawa hizo bure kwa baadhi ya wananchi.
Aidha alisema kuwa dawa hizo zitakazogawiwa bure zimenunuliwa na Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoani Pwani kwa gharama ya milioni 1.056,000 ili wananchi hao waondokane na malaria.
“Lengo la kampeni hii ni muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais dkt.John Magufuli alilolitoa wakati wa ziara yake katika kiwanda hicho Juni 22 mwaka jana ,ambapo aliagiza kila halmashauri Tanzania Bara kununua dawa hii na kuipulizia kwenye maeneo yenye mazalia ya mbu “alifafanua.
Hata hivyo mhandisi Ndikilo, aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kujitokeza kukunua dawa ili kupambana na mbu kwenye maeneo yao.
Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt Yudas Ndungile ,alisema licha ya takwimu kuonyesha ugonjwa wa malaria kushuka kimkoa lakini jamii iendelee kujikinga na kutumia njia nyingine kama dawa ,vyandarua ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Alielezeakuwa magonjwa yanayoongoza kwa sasa kimkoa ni magonjwa yanayotokana na mfumo wa hewa ,ikifuatiwa na malaria.
DktNdungile alisema ,mwaka 2016 ugonjwa wa malaria ulikuwa ukiongoza lakini kwasasa umeshuka na kuwa wa pili hivyo kuonyesha idadi ya vifo navyo kupungua.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.