Mkoa wa Pwani umepanga kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 178,024.699 zikiwa ni sh. Bilioni 32.36 za matengenezo na sh. Bilioni 145.662 za maendeleo ili kuboresha miundombinu ya barabara katika mwaka wa fedha 2019/20.
Taarifa ya hiyo ilitolewa na Wakala wa Barabara Kuu na za Mkoa (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa kilichofanyika machi 21, 2019. Kiasi hicho cha fedha kinajumuisha sh. Bilioni 94.671 za TANROADS na sh. Bilioni 83.353 za TARURA ambazo zitatumika katika matengenezo ya kawaida, matengenezo maalum, sehemu korofi, madaraja, kalavati na mifereji.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Assumpter Mshama akifungua kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa cha kupitia Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2019/20 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Kibaha Machi 21, 2019.
Katika ufafanuzi wake, Meneja TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi alibainisha kuwa taasisi yake itaboresha barabara zenye urefu wa kilomita 1,009.70 kati ya mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 1387.98.
Katika mtandao huo, Barabara kuu zina urefu wa kilomita 501.70 na zote ni za lami huku Barabara za Mkoa zikiwa na jumla ya urefu wa kilomita 886.28 (Tabaka la lami ni kilomita 34.13 na za changarawe zikiwa na urefu wa kilomita 852.15.)
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Bibi. Theresia Mmbando (aliesimama) akitoa maelezo ya awali katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa cha kupitia Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20. kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mjini Kibaha Machi 21.
Kwa upande wake mratibu wa TARURA Mkoa Mhandisi Lutufyo Mwakigonja alibainisha kuwa taasisi yake inahudumia mtandao wa Barabara wenye urefu wa jumla ya kilomita 3833.05, kati ya hizo, barabara za lami ni kilomita 37.17, barabara za changarawe ni kilomita 407.92 na barabara za udongo zina na urefu wa kilomita 3,387.96.
Awali, katika hotuba ya ufunguzi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo iliyowasilishwa kwa niaba yake na Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Assumpter Mshama aliwakumbusha wajumbe wa bodi hiyo kuwa moja ya majukumu yao kulingana na sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007 ni kupokea mipango ya ujenzi na matengenezo ya mwaka ya barabara na kuipitisha kwa lengo la kuhakikisha kwamba maeneo mbalimbali katika Mkoa yanafikika vizuri.
“Mipango na bajeti inayopitishwa visimamiwe na kutekelezwa kwa weledi na uadilifu mkubwa ili matokeo yake yaweze kuwa yenye tija kwetu sisi na kwa jamii nzima ya watanzania kwa ujumla ikizingatiwa kuwa fedha hizo ni za walipa kodi na sisi ndiyo tuliyopewa dhamana ya kuzisimamia” aliongezea Eng. Ndikilo.
Kwa pamoja kikao hicho kilipitisha mpango na bajeti hiyo.
Picha tatu za juu ni baadhi ya wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani wakipitia taarifa za Mpango na Bajeti za Wakala wa Barabara Kuu na za Mkoa (TANROADS) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mjini Kibaha Machi 21, 2019.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani Ndg. Ramadhani Maneno (aliesimama) akichangia hoja kwenye kikao cha kupitia na kujadili Mipango na Bajeti za TANROADS na TARURA kwa mwaka wa fedha 2019/20 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mjini Kibaha Machi 21,2019.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.