Kamati ya kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI imeuelekeza Mkoa wa Pwani kuandaa na kuwasilisha andiko lenye ombi maalum la kupewa fedha kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha miundombinu mbalimbali katika mkoa huo.
Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo leo Julai Mosi, 2024 kwenye kikao cha majumuisho mara baada ya kutembelea na kukagua baadhi ya miradi ya Miundombinu ya barabata inayotekelezwa na kusimamiwa na TARURA katika Mkoa huo.
Katika michango yao, wajumbe wa Kamati hiyo wamesema kuwa Mkoa huo ni wa Kimkakati, wenye Viwanda vingi na uwekezaji wa aina mbalimbali, hivyo ni vyema mkoa ukaandaa andiko litakalobeba mahitaji yote ya kiuchumi na kijamii (huduma, makazi, uzalishaji) ikiwa ni pamoja na kuandaa mazingira mazuri kwa kuweka michoro itakayoruhusu uwekaji miundombinu mipya wakitaja michache kuwa kama ya umeme, maji, gesi na mawasilano bila ya kuathiri iliyopo kwa ku ibomoa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Denis Londo amesema kuwa kutokana na mkoa huo kuwa na uwekezaji mkubwa hasa wa viwanda ambao una manufaa kwa Taifa ni vema wakaomba maombi maalumu ya fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara badala ya kuomba kidogo kidogo.
Awali, katika taarifa yake kwa kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameupatia Mkoa huo kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 1.23 za miradi mbalimbali za maendeleo huku TARURA na TANROADS wakiwa wamepewa Shilingi Bilioni 124.1.
Kamati hiyo imektembelea na kukagua barabara tatu ambazo ni ya kutoka barabara ya Morogoro kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha yenye urefu wa mita 300 iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 500, Visiga Zegereni kwenye eneo la viwanda kwa kiwango cha lami kilometa 12.5 kwa gharama ya shilingi bilioni 16.4 na umekamilika pamoja na ya ya Picha ya Ndege Boko Timiza kilometa 7.8 ambyo zimekamilika kilometa 1.2 awamu ya kwanza kwa shilingi milioni 950.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.