Serikali imetoa kiasi cha shilingi trilioni 1.19 kwa Mkoa wa Pwani kati ya Mach 2021 na Juni 2023 kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imeainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi - CCM.
Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye ni Kamisaa wa Chama hicho kwa mkoa huo Abubakar Kunenge, ameyasema hayo leo Novemba 22, 2023 kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho mkoa kilichofanyika kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ambayo imetaja miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo eneo la kwa Mfipa wilayani Kibaha, Kunenge amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambae amepeleka fedha nyingi mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, nishati, maji na miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, amesema chama kimeridhika na miradi iliyotekelezwa mkoani humo na kwamba serikali imetimiza matakwa yaliyopo kwenye Ilani ya CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Nae Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani Benard Ghatty amesema hadi sasa serikali imefikisha asilimia 98 ya utekelezaji wa miradi mkoani humo na kwamba sehemu iliyosalia ni ndogo ambapo wanaamini kuwa miradi yote itakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.
“Tumepitia, tumekagua na tumeona namna miradi ilivyotekelezwa katika maeneo mbalimbali mkoani Pwani, kuna sehemu ndogo tu ambazo zimesalia kukamilishwa, tunaamini miradi hiyo itakamilika na watanzania watahabarishwa miradi hiyo itakapokamilika," amesema Ghatty.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.