Makampuni 30 kutoka nchini China yameonesha nia ya kuja Mkoa wa Pwani - Tanzania , kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya mbalimbali za kiuchumi. Ujio wa makampuni hayo ni matunda ya safari ya timu ya baadhi ya viongozi na wataalam wa Mkoa wa Pwani waliokwenda nchini China hivi karibuni kujifunza masuala mbalimbali ya uwekezaji pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alieleza kuwa, kupatikana kwa wawekezaji hao kuja Mkoani Pwani ni mwendelezo wa uwekezaji mkubwa uliowekwa Mkoani Pwani na makampuni mengi kutoka nchi ya China.
Mhandisi Ndikilo alibainisha kuwa, viongozi na wataalam hao wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri ya Kibaha wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. Zuberi Samataba walitembelea nchini China kuona shughuli zinazofanywa na makampuni mbalimbali. “Timu hiyo ikiwa nchini China ilitembelea majimbo ya Jiangsu, Anhui, Guangdong na Majiji ya Shanghai na Beijing, waliweza kuona shughuli zinazofanywa na wawekezaji na kushiriki kongamano la wawekezaji na wafanyabiashara lillofanyika Beijing,” alisema Mhe.Ndikilo.
Mhe. Ndikilo pia ameziagiza Halmashuri zote za Mkoa wa Pwani kuendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili uwekezaji na ujenzi wa viwanda ili kutekeleza kwa upesi agizo la Serikali la ujenzi wa viwanda mia moja kwa kila Mkoa. Amezitaka Halmashuri hizo wakati zinapotenga maeneo maalum ya uwekezaji lazima zishirikishe kikamilifu taasisi wezeshi kuweka miundombinu muhimu ya maji, umeme pamoja na barabara ili maeneo yaweze kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Mbali na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji pia amezitaka Halmashuri pamoja na Watendaji wa Vijiji kuendelea kuwakumbusha na kuwaandaa wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji wa viwanda kama kujipatia ajira ili kujikwamua kiuchumi.
Awali akiwasilisha ripoti hiyo Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji Bw. Shangwe Twamala alisema pamoja na fursa nzuri za uwekezaji zinazotangazwa nchini, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinapelekea kuchelewesha mchakato wa uwekezaji. Aidha aliongezea kuwa ujumbe wa Pwani ulitembelea majimbo matano na kukutana na wafanyabiashara kutoka kampuni 108 za China na kueleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Mkoani Pwani ambapo tayari kampuni 30 kati ya 108 zimeshaonesha nia ya kuwekeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.