Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua kiwanda cha kutengeneza vioo cha Sapphire Float Glass Tanzania Limited, kilichopo kijiji cha Mkiu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambacho ni kikubwa kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini pia cha nne kwa nchi za Afrika.
Dkt. Samia amezindua kiwanda hicho leo Septemba 20, 2023 na kusema hatua hiyo ni mafanikio makubwa ya maboresho ya sera mbalimbali za uwekezaji ambazo zimesaidia kuwavutia wawekezaji.
Amesema hadi sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 750 za vioo kwa siku na kuajiri watu 1650 na kuongeza kuwa tayari soko la kuuza bidhaa hizo lipo nchini kwa asilimia 25 na 75 kikiuzwa nje ya nchi.
“Haya ndio matunda ya maboresho ya sera ya uwekezaji kwa kushirikiana na watalaam ambayo sasa tunaanza kuyaona, naamini nchi yetu itakuwa na wawekezaji wengi na tutafanya makubwa kwenye taifa hili kupitia sekta ya viwanda na biashara," amesema Rais Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha hayo, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na biashara imeandaa mfumo wa usajili kwa njia ya kielektroniki kwa wawekezaji ambapo watapata huduma za pamoja ikiwemo taratibu za upatikanaji hati za ardhi na leseni.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Zhen Yang amesema asilimia 80 ya malighafi yanayozalisha vioo hivyo yanapatikana nchini huku asilimia 20 pekee ndiyo kwa sasa yanatolewa nje ya nchi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashantu Kijaji, amemuomba Rais Dkt. Samia kutoa kibali cha uchimbaji wa madini aina ya Soda Ash ambayo yanapatikana eneo la Engaruka mkoani Arusha ili malighafi zote za kutengeneza vioo yapatikane hapa nchini.
Amesema kupatikana kwa kibali na kuboreshwa kwa miundombinu ya eneo yalipo madini hayo ya Soda Ash huko Engaruka kutasaidia kupunguza gharama za wawekezaji hao kuyafuata nje ya nchi na kuisaidia serikali kuongeza mapato.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amemueleza Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa mkoa huo una jumla ya viwanda 55 vilivyokamilika vinavyosubiri kuzinduliwa ili vianze kazi.
Kunenge amesema kuwa hadi leo, mkoa huo una viwanda 1525 ambapo kati yake vikubwa vikiwa 120 na vingine vikiwa ni vya kati na vidogo ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali na amewakaribisha wawekezaji kuendelea kuja kuwekeza kwa sababu fursa za uwekezaji katika mkoa huo bado zipo yakiwemo maeneo na mazingira yanavuyotia.
Ziara hiyo ya siku moja ya Rais Dkt. Samia mkoani humo pia imeshirikisha mawaziri mbalimbali na viongozi wa mkoa wa Pwani maalum kwa ajili ya uzinduzi wa kiwanda cha Sapphire Float Glass na kuzungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani humo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.