Timu za Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) na Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) za Mkoa wa Pwani zimekabidhi makombe ilivyoshinda kwenye mashindano ambayo yaliyomalizika Mkoani Tabora hivi karibuni.
Akipokea vikombe na tuzo hizo Katibu tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta na amewapongeza wachezaji hao leo ofisini kwake Mjini Kibaha ambapo timu za riadha zilifanya vizuri kwenye michezo ya riadha na kutupa mkuki kwenye michezo hiyo.
Amesema kuwa wachezaji hao wameuletea sifa mkoa wa Pwani na hiyo imetokana na kutumia vyema vipaji vyao na kuwa na nidhamu na kuzingatia yale waliyofundishwa na walimu wao.
"Nimeambiwa wachezaji tisa watashiriki mashindano ya sekondari kwa nchi za Afrika Mashariki yatakayofanyika hivi karibuni nchini Uganda nawasihi mlinde viwango vyenu,"amesema Mchatta.
Aidha amesema kuwa wanariadha hao waige mfano wa mchezaji wa riadha Steven Akwari ambaye licha ya kuumia lakini alikimbia na kumaliza mbio licha ya maumivu makali.
Naye Mkurugenzi wa Filbert Bayi Elizabeth Mjema amesema kuwa shule inaomba kusaidiwa baadhi ya mahitaji ikiwa ni pamoja na lishe, maji na matunda.
Mjema amesema kuwa inawagharamia baadhi ya wanafunzi wenye vipaji ambao wazazi wao hawana uwezo ambapo lengo la Filbert Bayi ni kutaka wanariadha kufanya makubwa kwenye mchezo huo.
Kwa upande wake mwalimu wa riadha wa timu za Filbert Bayi Ally Nyonyi amesema kuwa timu hiyo inafanya vizuri kutokana na kuwa na maandalizi mazuri na nidhamu.
Nyonyi amesema kuwa wao ni mabingwa kwa miaka mitatu mfululizo kwenye mashindano ya Umisseta na Umitashumta Taifa hiyo inatokana na kuwa na mazingira rafiki ya kufanyia michezo ambapo wanakuwa na muda mwingi wa kufanya mazoezi baada ya masomo.
Wakielezea jinsi walivyojiandaa na mashindano hayo huko Uganda wachezaji hao wamesema kuwa wamejiandaa vya kutosha na wanaamini watailetea nchi ushindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.