Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta amewaasa watumishi mkoani humo kujenga tabia ya ushirikiano na kuepuka migogoro au kuchongeana kazini ili kutoa huduma bora kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Mchatta ameyasema hayo leo Mei 15, 2024 wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao kilicholenga kusikiliza na kutatua kero na malalamiko na kupata maoni yao kwenye ukumbi wa Ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Amewaeleza kuwa iwapo kuna changamoto zinazowakabili kwa ujumla wao au kwa mmoja mmoja za kiutumishi ni vyema wakajenga utamaduni wa kufuatilia masuala yao kwa kuzingatia utaratibu usioleta kadhia.
"Hili linaenda sambamba na suala la utunzaji siri ambalo kwa watumishi ni jambo muhimu sana, haifai kutoa mambo ya ofisini nje bila kufuata utaratibu, hali hiyo inaweza kuwajengea sura na mambo yanayosababisha kujidharaulisha, na utumishi wa umma ni ufahari 'prestige," mtumishi wa umma ni mtu wa kufuata utaratibu wa hali ya juu," amesema Mchatta.
Amesisitiza suala la kila mtumishi kuwa na maandalizi mazuri, kuwahi kazini na kutekeleza majukumu yake kwa bidii ili kuleta tija katika eneo lake la kutekeleza majukumu yake kwenye halmashauri hiyo.
Aidha, katika kikao hicho, Mchatta amewapongeza watumishi hao kwa mchango wao wa kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo ambayo yatasaidia kutoa huduma kwa wananchi.
Pia katika kufanya vizuri kwenye matumizi ya mifumo ya mawasiliano ya Serikali ambapo halmashauri hiyo inashika nafasi ya pili kitaifa katika matumizi ya mfumo wa PEPMIS na akahimiza kuitumia mifumo hiyo kwa kuzingatia taratibu na maadili yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.