Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta ameupongeza Uongozi wa Cambridge Education pamoja na Shule Bora kwa miradi wanayoitekeleza hali iliyosaidia kupanda kwa elimu katika mkoa huo.
Kati ya mambo yanayotekelezwa kupitia mradi wa shule bora ni kuboresha ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo _mafunzo_ ya walimu kazini (MEWAKA) , ushirikishwaji wa wazazi,na utoaji wa chakula shuleni.
Hayo ameyasema wakati akifanya mazungumzo na ugeni kutoka Cambridge Education na Shule bora uliongozwa na Meneja Mkuu kutoka Kampuni ya MOTT MAC DONALD ,msimamizi wa Cambridge Education SIMON HARRIS na timu ya uongozi wa Shule Bora Tanzania ambao umekuja kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa mradi wa Shule Bora.
Mchatta amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha utoaji wa elimu bora ngazi zote ili kufikia malengo ya upatikanaji wa elimu kwa watoto wote nchini.
Amesema katika kufanikisha hilo, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo iliungana na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kupitia ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, vyoo, mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, ofisi za walimu, huduma za maji na usafi wa mazingira.
Vilevile ,Serikali inaunga mkono Maendeleo Endelevu ya Ualimu (TCPD) kupitia mafunzo ya walimu, kuandaa na kusambaza vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
‘Napenda kuchukua fursa hii kushukuru kwa msaada wa programu ya Shule Bora kwa mipango ya Serikali katika kuboresha ubora wa elimu chini ya maeneo mada ya ujifunzaji, ufundishaji, ushirikishwaji, na uimarishaji wa mifumo ili kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya kupata elimu" ’alisema Mchatta.
Mchatta ameeleza, Mkoa utaendelea kushirikiana na mradi wa Shule Bora ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora na kufikia malengo yao.
Nae Afisa Elimu Mkoa wa Pwani ,Sara Mlaki ameushukuru ugeni huo kutoka Uingereza ambao umeongozwa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya MOTT MAC DONALD na msimamizi wa Cambridge Education SIMON HARRIS na timu ya uongozi wa Shule Bora Tanzania ambao wametembelea Mkoani Pwani ili kuweza kuona masuala yanayotekelezwa na Shule Bora kwa ngazi ya shule za msingi ikiwamo ujifunzaji jumuishi na ushiriki wa viongozi.
Akiwasilisha taarifa fupi ya afua za mradi zilizotekelezwa hadi kufikia mwezi Mei 2024 Sara amesema, kupitia mradi wa shule bora ,mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi katika afua mbalimbali yalitolewa .
Sara ameeleza kuwa ,kupitia shule bora idadi ya wanafunzi wanaojua kusoma na kuandika imeongezeka na idadi ya wanafunzi wanajiamini imeongezeka.
"Na ongezeko hilo limetokana na walimu kupewa mbinu mbalimbali za kuwafundisha wanafunzi,'"
Pia ushiriki wa wazazi katika kuchangia masuala ya kuboresha mazingira ya shule na watoto kwa
ujumla umeongezeka.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya MOTT MAC DONALD na Msimamizi wa Cambridge Education nchini Uingereza, Simon Harris amesema amefurahishwa kuwepo nchini na kuona juhudi zinazofanywa na wasimamizi wa mradi wa Shule Bora sanjali na mbinu zinazotumika katika kufundisha watoto,na ushirikiano wa wazazi na walimu umekuwa mkubwa.
Mradi huo ulianzishwa april mwaka 2022, na kuzinduliwa Mkoani Pwani Wilaya Kibaha ambapo unafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia kitengo cha FCDO.
Shule Bora ni programu ya Serikali ya Tanzania ya kuboresha elimu ya awali na msingi kwa ufadhili wa mfuko wa UKaid wa Serikali ya Uingereza, unatekelezwa katika mikoa tisa
ya Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.