Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, leo ameuagiza uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) kutafuta na kufanyia kazi hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa Aprili 28, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Benki ya Ushirika.
Mhe. Kunenge alitoa agizo hilo wakati akifungua Mkutano wa 31 wa Mwaka 2024/25 wa CORECU uliofanyika katika Ukumbi wa Destiny, Kibaha kwa Mathias, Mkoa wa Pwani.
“Agizo langu kwenu, uongozi wa CORECU, ni kutafuta hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa Dodoma kwenye uzinduzi wa Benki ya Ushirika na kufanyia kazi maono yake ili kuendeleza Ushirika,” alisema Mhe. Kunenge.
Akiendelea, alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kwa matokeo ili kumuenzi Rais Samia, akibainisha kuwa mkoa wa Pwani hauamini katika kushindwa.
“Mhe. Rais haamini katika kushindwa. Mimi, mlezi wenu, siamini katika kushindwa, na Mkoa wa Pwani pia hauamini katika kushindwa. Tumpe heshima Rais kwa kufanya kazi zitakazowasaidia wananchi,” aliongeza Mhe. Kunenge.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa aliwapongeza viongozi wa CORECU kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwataka wasisite kuwachukulia hatua watu wanaokiuka sheria kwa kutorosha mazao kama korosho na ufuta.
“Korosho na Ufuta ni uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huu. Tusiwavumilie watu wanaotorosha mazao. Nimetoa maagizo kwa Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua kali kwa watakaobainika,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, alisema wilaya yake ipo katika hatua ya palizi za mikorosho na kuagiza maafisa ugani kufuatilia kwa ukaribu idadi ya mikorosho kwa kila kata, hatua inayosaidia kuifanya Kibiti kuongoza kwa uzalishaji wa zao hilo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mwenyekiti wa Bodi ya CORECU, Musa Hemed Mng’eresa, alisema kwa mwaka 2024/2025, chama hicho kimefanikiwa kuuza ufuta tani zaidi ya 13,000, mbaazi tani 295.7 na korosho kilo 19,989,228, na hivyo kufanikisha mauzo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 67.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa pembejeo, hali iliyochangia ongezeko kubwa la uzalishaji kwa wakulima.
Naye, Mrajisi Msaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bw. Mutaabazi, alisema mkoa huo una jumla ya vyama vya ushirika 202, ambapo 162 kati yake ni hai. Aliongeza kuwa wakulima 137,000 tayari wamesajiliwa kupitia mfumo wa MUVU.
Akizungumzia mafanikio, alisema vyama hivyo sasa vimeanza kutumia mifumo ya TEHAMA katika usajili na pia kujenga maghala ya kuhifadhi mazao yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.