Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ameagiza Idara ya Uzalishaji kumwandalia shamba la korosho ili aweze kulisafisha kama mfano kwa wananchi ambao hawasafishi mashamba yao, hali inayosababisha kupungua kwa uzalishaji wa zao hilo.
Agizo hili limetolewa lOktoba 10,2024, wakati wa mkutano wa wadau wa zao la korosho uliofanyika wilayani Mkuranga.
“Tunahitaji kuwa na uchungu na mashamba yetu ili kuongeza thamani na uzalishaji kwa ajili ya kukuza uchumi wetu. Ni kwa nini hatusafishi mashamba yetu? Na kwa nini hatupunguzi mikorosho mizee? Haya yote yanawezekana tukijipanga vizuri. Naagiza Mkuu wa Idara ya Uzalishaji anitayarishie shamba nitasafisha ili liwe mfano kwa wananchi,” alisema Mhe. Kunenge.
Aidha, Mhe. Kunenge aliagiza Bodi ya Korosho kuboresha zoezi la usajili wa wakulima ili kurahisisha utoaji wa pembejeo. Aliwataka wale wanaotoa taarifa zisizo sahihi kuchukuliwa hatua za kisheria. Alisisitiza kuwa majina ya wakulima yanapaswa kubandikwa kwenye mbao za ofisi za vijiji na vitongoji ili kuruhusu marekebisho ya taarifa kabla ya ugawaji wa pembejeo.
Pia aliwataka viongozi wa Vyama vya Msingi vya Awali (AMCOs) kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu makubaliano na maamuzi yaliyojadiliwa katika mkutano huo. Aliahidi kuandaa kikao na taasisi za kifedha ili kutatua changamoto ya wananchi kushindwa kupata mikopo na huduma za kifedha, jambo ambalo linachelewesha malipo kwa wakulima.
Mhe. Kunenge aliagiza mamlaka husika kuharakisha utoaji wa pembejeo kwa wakulima baada ya wadau kulalamikia ucheleweshwaji wa pembejeo, hali inayosababisha kupungua kwa uzalishaji wa korosho.
Aidha, alishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la korosho kwa kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bibi Hadija Nasri, alisema maendeleo ya zao la korosho yameimarika kutokana na maelekezo ya Mhe. Kunenge, na aliahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa pamoja na michango ya wadau yatatekelezwa ipasavyo.
Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho, tawi la Dar es Salaam, Dominica Mkangara, alieleza kuwa wamejipanga kuajiri vijana kupitia mpango wa BBT kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) kwa ajili ya kusaidia zoezi la usajili wa wakulima.
Bodi ya Korosho pia ilishauri matumizi ya mizani ya kidigitali, ambapo Meneja Mkuu wa Ushirika CORECU, Hamisi Mantawela, alisema mkoa wa Pwani unahitaji mizani 188, na tayari mizani 135 imesambazwa kwa AMCOs zote 102 zinazohudumia wakulima wa korosho mkoani humo. Aliahidi kushirikiana na Korosho Cooperative Joint Enterprises Limited (KCJEL) ili kuhakikisha mizani iliyobaki inapatikana kwa wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.