Mkuuwa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge ameanza kutekeleza mapendekezo na msimamo wa Serikali juu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyokithiri katika kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi wa kata hiyo, Kunenge alielezea kuwa nia ni kumaliza migogoro, kuipanga vizuri kata hiyo kwa kufuata sheria kwani haiwezekani Mapinga isishikike badala yake iwe inatajwa kukithiri kuwa na migogoro ya ardhi kuliko maeneo mengine nchini.
Alifafanua kuwa kuanzia februari 2 mwaka huu wa 2023 atafika Mapinga akiwa na orodha ya watu 20 wenye migogoro na wataenda mguu kwa mguu kwenye maeneo husika na kufanya Maamuzi ili kila mmoja aridhike na akaongeza kuwa zoezi hilo litaendelea huku kila mhusika akitaarifiwa juu ya mwenendo na maamuzi hadi watakapomaliza migogoro yote iliyofikishwa kwa Waziri.
"Mtakumbuka nilifika hapa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi (mb) kutatua kero za ardhi mkoa wa Pwani na alisema wazi kuwa takwimu inaonyesha hii ndio kata inayoongoza kwa migogoro ya ardhi nchini na akaunda kamati ya watalaam akiwemo Kamishna wa ardhi mkoa na mara ya pili nilikuja tena nikiwa na Waziri wa Ardhi wa sasa Mhe. Angelina Mabula ambapo alieleza kuwa Serikali imepokea mapendekezo ya kamati, na huo ndio msimamo wa Serikali," alifafanua Kunenge.
Aliongeza kuwa ameanza utekelezaji huo katika Kata hiyo ya Mapinga inao utofauti kulinganishwa na maeneo mengine kwani ni rahisi kutatua migogoro ya ardhi tofauti na kata hiyo ambayo migogoro yake ni migumu, ya muda mrefu na migogoro mingine tayari ipo mahakamani na akaeleza kuwa katika hatua hiyo inayochukuliwa na Serikali, wanatarajia kutenda haki lakini hatoweza kumvumilia yeyote atakayeleta chokochoko na kujiona yupo juu ya Serikali.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa aliweka bayana kuwa katika utekelezaji huo, hataingilia mahakama kwa maana ya maamuzi yaliyofanywa na mhimili huo na akaongeza kuwa endapo kutakuwa na masuala ya maadili kwa waliopewa dhamana ya kufanya Maamuzi yaani watendaji, basi ataarifiwe ili ashughulikie kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya mahakimu na atahakikisha kuwa haki inatendeka na kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama na amani inatawala.
Awali mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Halima Okash alisema kuwa kuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na kuwa kata hiyo inaongoza kwa uuzaji holela na uvamizi uliokithiri ambapo taarifa za migogoro hiyo zilishafika mkoani na ikaundwa timu ndogo kuangalia Utaratibu utakaotumika ili kusuluhisha na kutatua changamoto hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.