Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezielekeza Halmashauri za Mkoa huo kuzingatia matumizi ya mapato yenye kuleta tija kwa wananchi ili kuweza kukidhi matarajio yao ya kubadili hali za maisha yao kutoka kwenye uduni.
Kunenge ametoa maelekezo hayo leo Juni 19, 2024 alipokutana na kuzungumza na mabaraza ya maalum ya Rufiji na Kibiti yaliyokutana kwa nyakati tofauti kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali baada ya ukaguzi wa hesabu za fedha za mwaka 2022/2023 ulioishia juni 30, 2023.
Akiwa Rufiji kwenye Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, pamoja na kuipongeza halmashauri hiyo kupata hati safi, alisema wanaweza kuwa na hati safi lakini matumizi yao yasiwe na tija.
"Rufiji na halmashauri zingine zote za mkoa wa Pwani, hati safi sio 'issue' (suala) tena kwetu, sisi tunataka tija, hatuongelei tena hati safi, sisi tupo kwenye tija, kama wapo wanaopambana kupata hati safi, waache waendelee, sisi tunapambana na tija, amesema.
Katika mikutano hiyo, Kunenge ameyaelekeza mabaraza hayo kuhakikisha hoja zote zinapatiwa majibu na kuondolewa na kuepuka kuzalisha zingine mpya.
"Mwaka ujao kila mkuu wa Idara atakuwa anawasilisha hoja zake, awajibike nazo mbele ya kamati yako kwa sababu inaonekana wanapuuzia kuzishughulikia," ameagiza Kunenge.
Amewataka watendaji kuandaa mipango kazi ya kufunga hoja na maagizo ya Kamati ya Bunge na kuitekeleza huku akihadharisha wahusika wawe wanashughulikia mapema akisema "mtambue kuwa hoja zinazofika huku ni zile zinazokosa majibu ya ukaguzi toka kwa mkaguzi wa ndani ambazo kama mkizijibu hazifiki huku, zinazofika huku ni zinazoshindikana kufungwa na huo ni udhaifu ndani ya taasisi, na mtambue kuwa anaejibu si mkaguzi wa ndani, ni mkuu wa idara husika na timu yake ndani ya idara."
Katika mikutano hiyo Kunenge amesisitiza halmashauri kuongeza viwwngo vya mapato ili kuboresha huduma mwa wananchi, uzingatiaji wa Sheria, Taratibu na Kanuni pamoja na utekelezaji wa majukumu kwa umoja.
Mkuu huyo wa Mkoa pia ameupongeza uongozi na wakazi wa Rufiji na Kibiti kwa umoja, mshikamano na ushirikiano waliouonesha wakati wa changamoto ya Mafuriko yaliyoyakumba maeneo hayo mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta amewapongeza na kuwashukuru wana Rufiji na Kibiti wa namna walivyopambana kudhibiti madhara na athari za changamoto za mafuriko pamoja na kwa kupata hati safi huku akizisisitiza halmashauri kujikita zaidi katika kutozalisha hoja za ukaguzi.
Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rufiji Abdul Chobo amesema Halmashauri imepata hati safi baada ya ukaguzi wa hesabu za fedha za mwaka 2022/2023 ulioishia juni 30, 2023, Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali amejiridhisha kuwa kutokana na ushahidi wa vielelezo alivyopitia, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imepata hati safi.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ramadhani Shaha Mpendu ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa huduma wakati wa mafuriko na kwa kupatiwa fedha nyingi za miradi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.