Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amehamasisha wakazi wa mkoa huo kuwapeleka watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi mitano kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupata chanjo dhidi ya Surua na Rubella inayotolewa na serikali bila malipo.
Ameyasema hayo leo Februari 16, 2024 alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia umuhimu wa watoto kupatiwa chanjo hiyo na akaeleza kuwa ni muhimu watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi mitano kupata chanjo hizo ili kupata kinga ya kupambana na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
amesema kwa mkoa wa Pwani, watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 174,298 watapata chanjo katika maeneo mbalimbali kuanzia ngazi ya vituo vya huduma za afya, ngazi ya kaya kupitia kliniki inayotembea, mkoba, shuleni na maeneo mengine yaliyoanishwa.
“Zoezi la utoaji chanjo mkoani Pwani limezinduliwa februari 15 mwaka huu na litahitimishwa februari 18, imani yangu ni watoto wote kupatiwa chanjo hiyo, hivyo nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa serikali, dini, siasa na makundi maalum kusaidia kampeni hii ili watoto waliokusudiwa wapate chanjo,” amesema Kunenge.
Nayo Wizara ya Afya imewahakikishia wananchi kuwa chanjo ya Surua na Rubella ni salama na haina madhara yoyote kiafya hivyo ni muhimu watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wakapelekwa kupatiwa huduma hiyo ili kujikinga na maradhi ikiwemo nimonia, utapiamlo, ulemavu pamoja na kifo.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa mradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Georgina Joachim, kwenye uzinduzi wa chanjo uliofanyika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.
Amesema maneno yanayosemwa na wananchi kuhusu chanjo za Surua na Rubella kuwa na madhara sio kweli na kwamba hakuna taarifa yoyote waliyoipokea wizarani kwamba chanjo hizo zina madhara kwa binadamu.
Mganga mkuu wa mkoa, Dkt. Benedicto Ngaiza amesema Februari 15, zaidi ya watoto 50,000 walipatiwa chanjo ya surua na Rubella kutoka maeneo mbalimbali ya kutolea huduma mkoani humo na kuongeza kuwa muitikio ni mkubwa na huduma hiyo inatolewa bure.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.