Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kunenge alitoa wito huo Oktoba 2, 2024 wakati wa kikao cha majadiliano kati ya sekta binafsi (PPD) na serikali kilichofanyika leo katika Ofisi za Mkoa wa Pwani.
Akizungumza katika kikao hicho, Kunenge alisema ushirikiano huo utawezesha kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara, na hivyo serikali kuweza kuweka mazingira rafiki ya kukuza biashara na kuongeza uwekezaji.
"Lazima tushikamane kati ya sekta binafsi na serikali ili kuweza kujua wapi tunafanya vizuri na changamoto zilizopo ili kuhakikisha tunaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji," alisema Kunenge.
Pia aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanachangia kuongeza mapato ya serikali na kuboresha biashara zao kwa kutumia fursa mbalimbali zinazowezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji kwa kufanya mambo tofauti na waliyozoea.
Aidha, Kunenge aliwaasa wafanyabiashara na wawekezaji kufuata matakwa ya kisheria ili kuweka mazingira bora yanayowezesha serikali kutoa msaada stahiki.
Alisisitiza maafisa biashara kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya, akiongeza kuwa, "Tumia fursa unapopewa nafasi, na uhakikishe unachokifanya kinaonekana."
Kwa upande wake, Mwenyekiti (ni nani)wa Baraza la Biashara Mkoa wa Pwani alishauri serikali kutoa elimu kwa walipa kodi kabla ya kuwakamata na kuwatoza faini, akisema kuwa hatua hiyo inachangia wafanyabiashara wengi kupoteza mitaji yao na kusababisha biashara zao kufa.
Alipendekeza pia serikali kutengeneza huduma wezeshi mkoani, kama vile masoko, ili kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Jumuia ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka, alitoa wito kwa maafisa biashara wa mkoa na halmashauri kuwasaidia wakurugenzi kutambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kuziwasilisha kwa viongozi ili kuweka mazingira rafiki ya kutatua changamoto hizo na kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.