Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa huo, Mhe. Abubakar Kunenge, ameongoza kikao cha Baraza hilo kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kibaha, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia dhana ya 4R ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuimarisha uwekezaji wenye tija utakaoleta maendeleo chanya kwa wananchi.
Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Katibu wa Baraza hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Mkoa wa Pwani (TCCIA), Bw. Saidi Mfinanga, pamoja na wakuu wa wilaya, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, na wadau mbalimbali wa sekta binafsi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kunenge alieleza kuwa Mkoa wa Pwani unapaswa kuwa na mazingira bora ya kiuchumi yanayovutia wawekezaji, huku maendeleo yanayotokana na uwekezaji huo yakilenga kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
“Ili kufanikisha azma hii, Mkoa tayari umeanza utekelezaji wa mikakati kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, inayoongozwa na Prof. Kitila Mkumbo, kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vinavyomilikiwa na wazawa,” alisema Mhe. Kunenge.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka na kuwasilisha taarifa sahihi za mapato kutoka viwandani, hasa vile vinavyokuwa kutoka hadhi ya viwanda vidogo hadi vikubwa, ili takwimu hizo zisomwe katika Mkoa wa Pwani na kuchangia kwa usahihi katika pato la taifa.
“Takwimu za pato la taifa kwa mkoa zinatokana na taarifa rasmi za mapato kuwasilishwa kwa mamlaka husika. Lakini kwa sasa hatufanyi hivyo. Viwanda vinakua kutoka vidogo hadi vikubwa lakini mapato yake hayaonekani yanasomeka nje ya Mkoa. Hili linaturudisha nyuma kimaendeleo,” aliongeza Kunenge.
Mhe. Kunenge pia alitoa agizo la kuanzishwa kwa mabaraza ya biashara hadi katika ngazi ya kata ili kuibua changamoto halisi zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji, na kupanga mikakati sahihi ya kuzitatua. Aliwataka maafisa biashara kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kupata taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga, alisisitiza umuhimu wa utoaji wa taarifa sahihi za uzalishaji kutoka kwa wawekezaji na wamiliki wa viwanda ili kusaidia Serikali kubaini fursa za maendeleo ya kiuchumi.
Dkt. Wanga pia alishauri Mkoa wa Pwani kuandaa mkakati maalum wa kuendeleza sekta ya utalii, akisisitiza kuwa mkoa huo una vivutio vingi vya asili ambavyo bado havijatumiwa ipasavyo kama chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.