Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amesema hatowavumilia watendaji wa Serikali na chama ambao watabainika kuwa ndio chanzo cha migogoro ya ardhi katika kata ya Mapinga.
Mhe. Kunenge ameyasema hayo leo Agosti 10, 2022 wakati akipokea taarifa ya Kamati maalum iliyoundwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchunguza mgogoro wa ardhi uliopo katika kata ya Mapinga Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Kunenge amesema kuwa Serikali ya Mkoa haitamfumbia macho Mwananchi yeyote yule ambae nae atabainika kuwa ni chanzo cha mgogoro wa ardhi katika eneo hilo
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Kunenge amemuahidi Mhe. Mabula kuwa ataipitia kwa kina na wale wote ambao wametajwa kuwa ni chanzo cha mgogoro atahakikisha kuwa wanachukuliwa hatua za kisheria.
“Mhe. Waziri, nimepokea taarifa hii na naahidi kuwa nitaifanyia kazi na wale wote watakaobainika kuwa ni wahusika tutawachukulia hatua stahiki, hatutamuonea mtu wala hatutampendelea mtu tutatenda haki kwani hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Mhe. Kunenge.
Pia ameeleza kuwa hata kama ni viongozi wa chama cha Mapinduzi wametajwa kuwa nao ni tatizo basi atashughulika nao kwa mujibu wa taratibu za chama.
Akikabidhi taarifa hiyo, Waziri wa Ardhi Nyumba Maendelo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula amesama kuwa lengo la kamati hiyo ni kutatua migogoro katika eneo hilo pia na sehemu nyingine nchini.
Amesema kuwa kamati hiyo imefanya kazi kwa umakini zaidi na kuwahoji watu mbalimbali ambapo wamebaini kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni pamoja na wenyeviti wa vijiji na Vitongoji kuuza ardhi kiholela.
Waziri Mabula ametoa onyo kwa wenyeviti hao kuacha mara moja tabia ya kujipa madaraka ya kugawa ardhi bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Mhe. Mabula alifafanua kuwa mkoa wa pwani ni Mkoa wa mfano kitaifa katika suala zima la uwekezaji na kwamba Mhe. Rais anautizama kwa macho mawili, hivyo ni lazima kumaliza migogoro yote ya ardhi katika mkoa huo ili uwekezaji usikwamishwe.
Aidha ameezielekeza Halmashauri zote nchini kuanza kufanya ukaguzi wa mashamba pori na orodha hiyo ikabidhiwe kwake kwani kuwepo kwa mashmba pori mengi nacho ni chanzo cha migogoro.
Pia ametoa rai kwa wananchi wote kuwa kama wanahitaji maeneo waende Halmashauri husika ambapo ndipo atapata eneo sahihi na si kwa wenyeviti wala Watendaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.