Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe.Abubakari Kunenge, amesema hatokuwa tayari kumfumbia macho mtu yeyote atakaebainika kuhujumu Wananchi kwa kukwamisha utekelezaji wa bajeti na kuacha miradi kuwa viporo, hali inayosababisha kurudisha fedha Serikali kutokana na udhaifu huo.
Aidha, amekemea vikali tabia ya baadhi kujiingiza katika utekelezaji wa miradi kwania ya kujinufaisha wenyewe kwani kufanya hivyo kunawacheleweshea Wananchi maendeleo.
Kunenge alitoa rai hiyo katika kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022, mkataba wa lishe, miongozo ya elimu na tathmini ya ukusanyaji wa mapato kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Pwani, Kibaha.
Mkuu huyo wa Mkoa ambae alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alieleza kuwa Wananchi wanawapima kulingana na utatuzi wa kero zinazowakabili hivyo, lazima wajipime na wajipange kupata matokeo chanya.
"Kama utekelezi bajeti ,utakuwa unakwamisha huduma za maendeleo, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anatupatia mafungu ya fedha za kutosha, hatuwatendei haki wananchi, Tunaletewa fedha halafu mwisho wa mwaka miradi haitekelezwi na fedha zinabaki" Inapaswa tuwajibishane, Hatuwezi kuwaacha. Alisisitiza Kunenge.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Zuwena Omary alishukuru kwa kupata ushirikiano wa kutosha tangu kufika Mkoani hapo na kusisitiza kufanya kazi kwa timu na ushirikiano ili kufikia maendeleo yanayokusudiwa na Mkoa.
Nae Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Rukia Muwango alieleza kuwa, Mwaka wa fedha 2022/2023 Mkoa wa Pwani fungu 71 umeidhinishiwa bajeti ya Sh. 335,110,456,000 kati ya kiasi hicho Sh. 206,063,824,000 ni ruzuku ya matumizi ya kawaida, Sh. 80,568,294,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Sh. 48,478,338,000 za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Aliendelea kufafanua kwamba, bajeti ya Mkoa wa Pwani kwa mwaka 2022/2023 imeongezeka kwa Sh. 36,279,573,000 sawa na asilimia 12.14 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2021/2022. Ongezeko hilo limetokana na mishahara kwa asilimia 19.38, matumizi mengineyo (OC) asilimia 21.82 , fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo asilimia 9.44 na mapato ya ndani ya Halmashauri asilimia 23.33.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.