Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge ameelekeza taasisi wezeshi Mkoani humo kuwa tayari mda wote kutatua changamoto zozote zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mradi wa Kongani ya SINOTAN iliyopo Wilayani Kibaha.
Kunenge alitoa maelekezo hayo leo Mach 6, 2023 alipotembelea na kukgua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na mapendekezo ya mwekezaji ili kufanya maboresho yenye tija kwa pande zote mbili kwa maana ya Serikali na Mwekezaji
Akifafanua baadhi ya miradi inayotekelezwa na serikali kuwezesha Kongani hiyo ambayo aliitaja kuwa ni uwekezaji mkubwa mkoani humo itakayokuwa na viwanda zaidi ya 300 ambazo kwa pamoja zitatoa ajira 100,000, Kunenge alisema tayari Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani humo wanatekeleza Mradi wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 ambao utakapokamilika utamaliza tatizo la uhaba wa maji hasa katika wakati huu wa Ujenzi na DAWASA wanajipanga kutekeleza mradi mkubwa utakao maliza tatizo la Maji katika eneo hilo na la Uwekezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha huku TANESCO wakiboresha hali ya umeme kutoka Megawat 10 hadi 50 na kuwa kufikia mwezi Juni tatizo katika huduma hizo litakuwa limeisha.
Aliendelea kusema kuwa Serikali itakamilisha ujenzi na uwekaji wa miundombinu yote muhimu kwenye kongani ikiwa ni pamoja na barabara ya njia nne ya zege kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam - Morogoro kupitia bandari kavu ya kwala hadi eneo la Kongani hiyo.
"Pwani tunaendelea kuwa mstari wa mbele kwa uwekezaji wa viwanda na mkoa huu ndio mfano mzuri, eneo hili litakuwa kubwa kwenye uwekezaji, wanaoanzisha Kongani kwenye maeneo mengine waje kujifunza hapa mpangilio na mambo mengine," alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kuwa kufuatia mazungumzo ya pamoja na wataalamu kutoka kwenye taasisi wezeshi, kuanzia sasa watakuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara kutatua vikwazo vinavyoweza kujitokeza kwenye mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
"Tumekubaliana hizi taasisi zinazohusika na kuunganisha huduma kwenye hii kongani zikutane na uongozi wa SINOTAN ili waonyeshwe ramani ya mpango wa ujenzi, hii itasaidia kutoharibu maendelezo yaliyokamilika wakati wa kuweka miundombinu mingine na kupunguza gharama," alisema Kunenge.
"Lengo la Serikali chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan ni kuwarahisishia wananchi maisha kwa njia mbalimbali ikiwemo kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa ajira hivyo kama viwanda hivyo vitaanza kazi nidhahiri vitakuwa vinajibu changamoto hizo," aliongeza.
Awali, Mwenyekiti wa Kongani hiyo Janson Huang alisema ifikapo June mwaka huu kituo cha huduma kitakuwa kimekamilika na kiwanda cha kwanza kitaanza kazi na kwa kuwa katika hatua za awali, takriban ajira 5000 zinatarajia kutolewa kwa watanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.