Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, amewataka wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa huo kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara unafanyika kwa ufanisi na kulenga maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Akizungumza Machi 4, 2025, katika kikao cha bodi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Kunenge alisisitiza kuwa juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara zinapaswa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
Kazi yetu ni kutatua changamoto kwa kuhakikisha tunalenga vipaumbele sahihi na kutekeleza miradi kwa ufanisi. Hatupaswi kutumia muda wetu kulalamika bali kutafuta suluhisho na kuweka mikakati thabiti kwa kuzingatia rasilimali zilizopo, alisema Mheshimiwa Kunenge.
Katika kikao hicho, wajumbe walipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa robo tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, aliwasilisha taarifa ya miradi inayoendeshwa na TANROADS, huku Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Leopold Runji, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TARURA.
Wajumbe wa bodi walikubaliana kuwa usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa na serikali na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutasaidia kuboresha miundombinu ya barabara na kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.