MKuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amewataka wananchi wa Kitongoji cha Sanzale kilichopo Kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyokuhakikisha wanalipia fidia ya eneo walilovamia kama yalivyo makubuliano na Familia hiyo inayomiliki eneo hilo.
Kufuatia mgogoro huo ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amefika katika eneo hilo mapema April 22,2022 kwa ajili ya kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo na kutoa maagizo mbalimbali.
Miongoni mwa maagizo ya Kunenge kwa wananchi hao ni kuhakikisha Kila mwananchi aliyejenga katika eneo hilo kuwa alipe fidia kama walivyokubaliana badala ya kuvunja na kuondoka
Aidha , Kunenge amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo Zainabu Abdallah kuhakikisha anaendesha msako wa kuwakamata matapeli wote waliohusika katika eneo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha Amesema kuwa nchi hufanyakazi kwa kuzingatia mihimili yake mitatu ikiwemo Bunge,Mahakama na Serikali huku akisema mihimili hiyo haiingiliani maamuzi yake.
Amesema kuwa,jambo ambalo limeamriwa na Mahakama hakuna anayeweza kutengua wala kuingilia isipokuwa hatua nyingine ya Kimahakama(Rufaa) na kwamba kinachotakiwa ni utekelezaji wa Mahakama .
Ameongezea kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo katika kuwasaidia wananchi na ndio maana amefika eneo hilo kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia taratibu na misingi ya kisheria.
"Kuna mambo yanatatuliwa kiutawala na Kama mnadhani kuna mtendaji anakiuka utaratibu basi naweza kulishughulikia lakini jambo la Mahakama lazima liheshimiwe ,"amesema Kunenge
"Naishukuru familia ya marehemu kwa kugoma kubomoa nyumba za wananchi hawa lakini namuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia kwa karibu ili wakishakubaliana watu hawa wafanyiwe mpango wa kupewa hati za umiliki,"amesema
Kunenge,ameendelae kusema mbali na maagizo hayo lakini pia atafanya kikao na baadhi ya wawakilishi wa wananchi, msimamizi wa mirathi,familia na Mkuu wa Wilaya ili kuona namna ambavyo wananchi hao watalipa kwa utaratibu maalum na wenye kufaa.
Amesema kuwa,baada ya utaratibu huo kukamilika wananchi hao watapata huduma zote muhimu ikiwemo maji na umeme huku akiwasisitiza wananchi kufuata sheria na taratibu pale wanapotaka kununua na hata kujenga nyumba zao.
Nae msimamizi wa mirathi hiyo Salim Mgombeo,amesema kuwa anachotaka yeye ni kuwa wale waligoma kulipa waondoke lakini waliokubali kulipa wabaki na kwamba mgogoro huo ni mkubwa.
Baadhi ya Wananchi hao akiwemo Amina Azizi na Hassan NG'anzi,wamesema wao wapo tayari kulipa na wameomba Serikali iweke utaratibu maalum ambao utawawezesha kulipa bila usumbufu .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.