Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe Abubakar Kunenge amewataka wananchi wote Mkoani hapa kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi zilizoweka.
Pia ameiomba Mahakama na watoa maamuzi kutoa maamuzi kwa kuzingatia sheria ya nchi bila kufanya uonevu wowote.
Rai hiyo ameitoa Februari I, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai,” ambapo kimkoa yamefanyika wilayani Kibaha katika Viwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani.
Kunenge amesema kuwa haiwezekani kuwa na utawala bora kama hakuna uzingatiaji wa utawala wa sheria na kuwa nchi hii inaongozwa kwa taratibu na kanuni za kisheria na hakuna aliye juu ya sheria hivyo watu wote wanapaswa kufuata sheria.
Ameeleza kuwa wananchi wengi hawafahamu vizuri masuala ya kisheria hivyo amewaomba wananchi hao kufuatilia kwa makini elimu za kisheria zinazotolewa na vyombo vya Habari huku akiziomba taasisi zinazojihusisha na masuala ya kisheria kutoa huduma ya elimu ya masuala hayo kwa wananchi.
RC Kunenge pia ameziasa mahakama kufanya maamuzi katika mashauri mbalimbali badala ya kukaa nayo kwa muda mrefu ambapo huleta sintofahamu kwa wananchi.
Ameeleza kuwa haki inaleta ustawi kwa jamii hivyo mwananchi anatarajia kupata haki yake kwa wakati na akichelewa yeye anahukumu kuwa mahakama haitendi haki ingawa inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria.
“Mkoa huu tunadhamana kubwa ya kumsaidia Rais wetu, hivyo kama sisi ni watu wa kufanya maamuzi tunapwa kutenda haki, tusimuonee mtu wala tusimpendelee mtu,” amesema Kunenge,“ na akaongeza kusema "tunafahamu mahakama inafanya kazi kubwa sana ya mfumo lakini sasa wananchi mifumo hiyo baadhi yao hawaifahamu hivyo elimu bado inahitajika kwa wananchi ili wasuje kuona wamekosa haki zao.”
RC kunenge amemalizia kwa kuwataka wanasheria wa kujitegemea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia kiapo chao ili kuweza kuleta haki na kuacha kufanya kwa maslahi yao binafsi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.