Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa huo Abubakar Kunenge ameeleza kuwa Mkoa wake umejipanga kuendelea kutoa Elimu ya kuhamasisha Wananchi wote ili waweze kushiriki kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022.
RC Kunenge ameyasema hayo leo Julai 20, 2022 alipotembelea kituo cha Mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya Mkoa ambako jumla ya makarani Wakufunzi 200 kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani wanapatiwa Mafunzo hayo katika Ukumbi wa Destiny Kibaha kwa Mathias.
Akizungumza na Wakufunzi wanafunzi hao, RC Kunenge amewaeleza kuwa ili sensa iweze kufanikiwa, inatakiwa kuzingatia mambo muhimu ikiwemo kuhakikisha utayari wa Wananchi kushiriki zoezi kwa hiari yao na kuhakisha uwezo wa kusimamia na kuendesha zoezi zima kwa maana ya vifaa na Wataalamu.
"Kama tunauwezo mzuri lakini Wananchi hawajajitokeza hatuwezi kufanikiwa" Ameeleza Kunenge.
Amefafanua kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa Rasilimali watu itakayoshiriki kwenye shughuli hiyo inapata elimu na kwenda kufundisha wengine na akasema, "Kazi yenu ni muhimu sana ninyi hapa ndio Mnaoweza kukwamisha au kufanikisha zoezi hili, hivyo zingatieni kanuni na Taratibu wakati wa Utekelezaji wa zoezi la Sensa kwani dhamana mliyonayo ni kubwa hivyo sitarajii kuona kuwa kati yenu kuna watu watakao jitoa kwenye zoezi hilo katikati ya mafunzo na baada ya kupata mafunzo.”
Amewasisitiza wakufunzi wanafunzi hao kujifunza na kuelewa ili wakawapatie wengine mafunzo sehemu nyingine katika Mnyororo wa majukumu ya Sensa na akawaeleza kuwa ikiwa hawatatenda sawa, kuna uwezekano wa kuharibu zoezi hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.