Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa kutumia rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao.
Kunenge ameyasema hayo leo Novemba 20, 2023 akifungua mafunzo ya siku mbili kwa maafisa tarafa na watendaji wa kata 152 kati ya 160 wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani yanayofanyika katika kata ya Msangani Halmashauri ya Mji Kibaha.
Amesema mafunzo hayo yana tija kubwa kwa watumishi hao ambao moja kwa moja wanaishi na wananchi hivyo ni rahisi kufahamu vikwazo vinavyowakabili na kuwatatulia.
Kunenge ametumia nafasi hiyo kuwafundisha watumishi hao namna ya kuwa watumishi bora wenye kuzingatia sheria, kanuni za utumishi wa umma na akasema anaamini baada ya mafunzo hayo watafanya vizuri zaidi.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa watumishi hawa kujengewa uwezo ili kuwa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi, nimekuwa nikitumia nafasi yangu kuwapa maarifa watumishi hawa kwa lengo la kujibu changamoto za wananchi kwa vitendo,” amesema.
Ameongeza kuwa anaamini baada ya mafunzo hayo wananchi watatatuliwa changamoto zao kwa wakati na kwa weledi unaotakiwa.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa, Ibrahim Minja amesema ni awamu ya pili mafunzo ya aina hiyo kutolewa ambao kwa sasa yanafanyika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Mtwara, Singida, Dodoma na Tabora na kwa awamu ya kwanza yalitolewa mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Katavi.
Amesema mafunzo hayo yana mada 15 ambazo zitafundishwa na wataalam kutoka Chuo cha Hombolo na Utumishi wa Umma ambao watawafundisha namna ya kuzingatia misingi ya kazi ikiwemo la maadili ili kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Minja ameongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kupata matokeo mazuri ya kile walichokifundisha kwa wananchi ambao watafurahia huduma.
“Mafunzo haya yana lengo la watumishi hao kukumbushwa wajibu wao nafasi zao kufahamu miongozo mbalimbali ya utumishi ili kuboresha maisha ya watanzania,” amesema.
Baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo akiwemo Jane Mwanantwa Afisa Mtendaji kata ya Kawawa wilaya ya Kibaha, amesema yana umuhimu kwa sababu wanakumbushwa wajibu wao pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wananchi wanaowahudumia.
Afisa Mtendaji wa kata ya Msangani, Benjamin Mputtu amesema wameongezewa maarifa ambayo yatawasaidia kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.