Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaelekeza Viongozi wa Wilaya, Halmashauri na Wakala wa Huduma za Misitu mkoani humo kuzingatia utunzaji wa misitu iliyohifadhiwa kwa kuzuia uharibifu wa misitu ili kuhifadhi mazingira.
Maelekezo hayo ya Mkuu wa Mkoa yametolewa kwa niaba yake Mjini Kibiti April 9, 2024 katika siku ya upandaji miti kimkoa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo.
Amesema kuwa viongozi wa Vijiji wanapogawa au kuuza maeneo wahakikishe hawaingilii yale yenye misitu hata kama hayajahifadhiwa kisheria.
"Zuieni uchomaji mkaa, uvamizi wa Mifugo, uchimbaji wa michanga, kokoto kilimo na kuweka makazi katika maeneo hayo kwani ongezeko la watu na ukosefu wa nishati ni moja ya mambo yanayotoa msukumo wa mahitaji ya mazao ya misitu ikiwemo kuni, mkaa na maeneo ya makazi hivyo kusababisha kuongezeka kwa ukataji na ufyekaji wa misitu," amesema.
Katika maelekezo hayo amesema kuwa endapo Serikali za Vijiji, Wilaya, Halmashauri na Taasisi nyingine zitasimamia maelekezo hayo itaimarisha ulinzi na usimamizi wa misitu kwenye maeneo yao.
Pia amesisitiza kuwa kila Halmashauri za mkoa huo ziwe zinapeleka taarifa ya maendeleo ya miti iliyopandwa mwaka kila mwaka na kueleza idadi ya miti ikiwa ni pamoja na mingine iliyokufa.
Kanal Kolombo amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023, mkoa wa Pwani ulipanda miti 8,876,640 na katika msimu huu wa 2023/2024 miche 10,436,494 imezalishwa na inaendelea kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
"Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani nawasilisha maelekezo haya ya kila Halmashauri kuhakikisha wanafikia malengo ya Serikali kupanda miti Milion 1.5," amesema Kanali Kolombo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Kanda ya Mashariki, Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Shabani Kiula amesema majukumu waliyonayo ni kuhakikisha misitu inaendelea kuhifadhiwa na wanaendelea kutoa miche aina mbalimbali bure ili watanzania wapate na kupanda kwenye maeneo yao.
Naye Afisa misitu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Pierre Ntiyamagwa amesema pamoja na upandaji miti pia wanakabiliana na uharibifu wa rasilimali misitu na uhifadhi wa mazingira.
"Hatua zulizochukuliwa ni pamoja na kufanya doria zinazoendesha na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, kuongeza mwamko wa uanzishwaji wa vitalu vya niche na upandaji miti kwenye Asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali," amesema.
Ameongeza kuwa vipo vikwazo vinavyoikabili rasilimali ya misitu akivitaja kuwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salam ambalo husababisha mahitaji makubwa ya kuni na mkaa na hivyo kuongezeka kwa ukataji na ufyekaji misitu na mapori mkoani humo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.