Uongozi wa Mkoa wa Pwani, umeagiza wale wote wanaovuna mazao ya misitu bila kufuata sheria kuondoka mara moja kwenye hifadhi za Misitu na vyanzo vya maji mkoani humo.
Agizo hilo limetolewa leo Novemba 25, 2022 na Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Kmati ya Usalama mkoa pamoja na Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki na wilaya ya Kibaha, Mhe. Kunenge alitahadharisha kuwa yeyote atakayekaidi na kukiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Alitoa tamko na maagizo hayo ya utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji na uvunaji wa raslimali za misitu, kwa waandishi wa habari Mkoani Pwani.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi mbalimbali katika Mkoa huo kuanzia ngazi ya chini pamoja na wakuu wa wilaya kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na akawaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji.
"Kuna uvunaji holela wa misitu kwenye Maeneo ya vijiji na uharibifu wa vyanzo vya maji kinyume cha sheria, jambo hili lisiendelee tena kwasababu tunafahamu misitu hii ni maliasili ya Taifa na inavunwa na kutunzwa kisheria," alisema Mhe. Kunenge.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kunenge alikemea ufugaji holela wa mifugo na akasema kuwa mkoa umeanza kutambua na kutenga maeneo kwa ajili ya kuwapa wafugaji kuhifadhi mifugo yao na akawataka wafugaji kuanza kufuga kwa tija kwa kubakiza mifugo michache wanayoweza kuimudu.
"Mifugo isizurure ovyo, sisi kama mkoa kwa hatua ya sasa tunatenga maeneo ya wafugaji, wafugaji lazima wavune mifugo ili kubaki na mifugo michache yenye tija na wanapaswa kujuwa kuwa ardhi haiongezeki," alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.