Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka wakulima na wataalamu kuhakikisha wanaongeza mnyororo wa thamani ya zao la korosho ili lilete tija.
Kunenge aliyasema hayo Wilayani Mkuranga kwenye mkutano wa wadau wa korosho wa mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa kwa msimu uliopita mkoa ulifanya vizuri ambapo korosho daraja la kwanza ilikuwa ni asilimia 72 ambapo jumla ya tani 16,000 zilivunwa ikilinganishwa na msimu wa nyuma ambapo zilivunwa tani 7,000 huku daraja la kwanza likiwa asilimia mbili.
"Mwelekeo siyo mbaya nataka tuende mbele kwani tayari tuna asilimia 72 tunapaswa kushirikiana ili tusonge mbele siyo kurudi nyuma kama ni mtaji tayari tunao," alisema Kunenge.
Alisema kuwa ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali kitaifa ya kuvuna tani 36,000 ifikapo 2025 ambapo hiyo itafikiwa endapo changamoto zilizoonekana msimu uliopita zitafanyiwa kazi mapema.
"Tuhakikishe tunazingatia matumizi ya viuatilifu kwa wakati, kufanya palizi na kutumia miche bora na ile ya zamani waikate matawi ili ichipue upya kwa kupandikiza vikonyo,"alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa mkoa wa Pwani umejipambanua kuboresha sekta ya kilimo kuanzia kwenye korosho na ufuta pamoja na mazao mengine ya biashara na asingependa maneno na kuona kiwango kinashuka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.