Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhe Abubakar Kunenge amewaagiza wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kusimamia sheria katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Kunenge alitoa maagizo hayo alipokuwa katika hafla fupi ya kuwaapisha wakuu wa Wilaya ambapo amewasisitiza kusimamia sheria asiwepo mtu wa kupendelewa wala atakayeonewa.
Pia aliwataka wakazi wa Mkoa huo kuheshimu sheria huku akionya wenye tabia ya kuvamia maeneo na kuyauza kuacha tabia hiyo.
" Baadhi ya migogoro ipo katika maeneo ambayo yana hatimiliki za ardhi, kama shamba utaratibu upo utafuatwa na mamlaka zinazohusika" alisema Kunenge.
Kunenge pia akiwasisitiza wakuu hao wa Wilaya kutatua kero za wananchi ambazo zipo ndani ya uwezo wao na zilizo nje wahakikishe wanazifahamu kabla ya kuzifikisha mamlaka za juu.
"Kama kila mmoja atasimamia majukumu anayotakiwa hakutakuwa na kero kwa wananchi siamini katika uongozi wa mtu mmoja tushirikiane na kila mmoja awe tayari kujifunza" alisema.
Aidha aliwataka kushirikiana na Halmashauri kuongeza mapato na kusimamia miradi ikamilike kwa wakati.
Aliwataka pia kila mmoja kusimamia uainishaji wa maeneo ya uwekezaji lakini pia maboresho ya madaftari ya makazi.
Nae kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri aliahidi kutekeleza maagizo ya mkuu wa Mkoa huku akisema ataanza kwa kukaa na wananchi kwenye maeneo ya migogoro kuitafutia ufumbuzi.
Wakuu wilaya waliopishwa ni pamoja na Col. Ahmed Abas Ahmed Mkuu wilaya ya Kibiti, Mhe. Khadija Nassir Ali mkuu wa wilaya ya Mkuranga na Mhe. Nickson Simon John Mkuu wa wilaya ya Kisarawe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.