Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezisisitiza timu za Menejimenti za Halmashauri katika mkoa huo kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa jithidada kubwa na kudhibiti mianya ya upotevu ili kuiwezesha serikali kutoa huduma kwa wananchi.
Kunenge ametoa msisitizo huo leo Februari 12, 2024 alipokutana na timu za menejimenti za halmashauri za Kibaha Mji, Kibaha DC, Bagamoyo na Chalinze ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI aliyeelekeza wakuu wa mikoa katika maeneo yao kukutana na timu hizo.
Maagizo ya Waziri wa TAMISEMI yameelekeza wakuu wa mikoa kufuatilia hali ya vipaumbele katika wakati huu wa maandalizi ya Mpango na bajeti ya 2024/2025 vinavyojibu hoja za wananchi, mikakati ya ukusanyaji mapato na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Maagizo mengine yameelekeza halmashauri kutoa taarifa zao za upelekaji fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo, usimamizi miradi ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaoakisi kiasi cha fedha kilichotolewa, taarifa ya utoaji wa asilimia 10 za mapato ya ndani kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu pamoja na mikakati ya utekelezaji taarifa za hoja za Mdhibiti na Mkagunzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) na za Kamati ya Bunge LAAC na (TAMISEMI).
Katika mkutano wa kwanza kati yake na Menejimeti za Halmashauri za Kibaha TC na Kibaha DC kwenye ukumbi wa mikutano wa Kibaha TC na baadae za Bagamoyo na Chhalinze kwenye Ukumbi wa mikutano ofisi za halmashauri ya Bagamoyo, Kunenge amewaelekeza kufanya kazi kwa uwezo wao wote ili waweze kuleta matokeo chanya yenye kujibu changamoto za wananchi.
"Kila mtu atekeleze majukumu yake, tunatakiwa tukusanye mapato mengi zaidi kadri inavyowezekana ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi ambao wanataka kila kitu cha kimaendeleo kinatekelezwa, tukijipanga vizuri tutafanikiwa kwani uwezo wetu ni mkubwa kuliko changamoto zinazotukabili," amesema.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rshid Mchatta ameeleza kuwa tayari ameshafanya kikao na wakurugenzi wote wa halmashauri mkoani humo kuweka mikakati ya pamoja itakayoweza kufanikisha utoaji bora huduma kutokana na kuongeza jitihada kuharakisha maendeleo kwa kuboresha ukusanyaji mapato na kuweka mifumo mizuri ya usimamizi wa maelekezo ya serikali.
Nazo Menejimenti hizo zimeahidi kuwasilisha mikakati yao ya utekelezaji wa maelekezo hayo kikamilifu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.