Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, leo Februari ,2025 amezindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) katika viwanja vya Maili Moja, Wilaya ya Kibaha.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria bure kuhusu masuala ya ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia, na migogoro ya ardhi.
Naomba mjitokeze kwa wingi ili kupata msaada wa kisheria, kwani hii ni juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi bila gharama yoyote,†alisema Mhe. Kunenge.
Kampeni hii itafanyika kwa siku tisa katika halmashauri zote na wilaya saba za mkoa wa Pwani, ambapo wananchi watapata elimu na msaada wa kisheria. Mhe. Kunenge amewahimiza watumishi na wadau wa sheria kutumia kipindi hiki kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, alibainisha kuwa kampeni hii tayari imezinduliwa katika mikoa ya Mwanza na Lindi, na leo Februari 24, imezinduliwa Pwani na Mbeya. Ameongeza kuwa ifikapo Mei 2025, kampeni itakuwa imetekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaid Hamis, amewasihi wananchi kufika kwenye vyombo vya sheria wanapokutana na changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, na haki za binadamu, ili kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.