Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ameziasa taasisi zinazosimamia sheria kutoingiza baadhi ya mashauri kwenye taratibu za usuluhishi akitaja mfano wa zinazohusu kuwapa mimba Wanafunzi.
Mhe. Kunenge aliyasema hayo leo Febuari Mosi, 2023 wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria nchini ambayo Kimkoa yamefanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha.
Akizungumza kwenye Hafla hiyo Mhe. Kunenge pia amezisisitiza taasisi hizo kuwapa Wananchi Elimu ya taratibu za kimahakama ikiwa ni pamoja na zinazohusu kukata rufaa katika kutafuta haki zao.
"Nchi yetu inamihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, pamoja na kuwa mihimili hii inajitegemea lakini ni lazima zishirikiane na watendaji katika mihimili hiyo watumbue kuwa kipaumbele cha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha Demokrasia na Utawala wa Sheria" alifafanua Kunenge.
Mkuu huyo mkoa alibainisha kuwa yeye kama Kiongozi wa Serikali ya Mkoa, anaheshimu maamuzi ya Mahakama lakini anayo nafasi ya kushughulikia baadhi ya masuala kwa nafasi yake ya Uwenyekiti wa maadili ya mahakimu.
Akizungumzia Kauli mbiu ya Siku hiyo ya Umuhimu wa Utatuzi Wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza Uchumi Endelevu, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya kibaha Mhe.Joyce Mkhoi pamoja na kumshukuru Mhe. Kunenge kwa kuwezesha kupatikana eneo la kujenga Mahakama Kuu, pia alieleza kuwa Mahakama inaendelea kutoa kipaumbele kwenye usuluhishi kwa kesi za jinai na madai na akaviomba vyombo vya habari kutoa elimu kwa Wananchi faida za usuluhishi Ikiwemo kuokoa muda na wananchi kuendelea na shughuli za Uzalishaji Mali na akaeleza kuwa changamoto wanayokabiliana nayo ni upungufu wa Wataalamu wa usuluhishi kwa ngazi ya Kata na Wilaya.
Katika maadhimisho hayo, akisoma hotuba ya kwa niaba ya Mawakili wa Kujitegemea TLS , Pwani, Wakili Julieth amesema wanaamini katika usuluhishi kutatua Migogoro mbalimbali badala ya kukimbilia mahakamani na akasema kuwa Usuluhishi unatatua Migogoro, kukuza undugu na kuongeza wigo wa upatikanaji haki kwa gharama nafuu.
Naye Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Pwani Wakili Mkunde Mshanga akitoa Salaam kwenye hadhara hiyo alieleza kuwa kauli mbiu ya Utatuzi wa Migogoro kwa usuluhishi ni takwa la Msingi kwa mujibu wa Katiba na kuwa wataendelea kusimamia maelekezo ya Serikali ya kumaliza Migogoro kwa njia ya maridhiano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.