Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka watumishi waliochini yake Mkoani humo kutosubiri changamoto za wafanyabiashara ziwakute kwenye vikao ndipo watafute njia za kuwasaidia na badala yake wajenge utaratibu wa kuwafikia Ili kuzitambua na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo February 3, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la biashara la mkoa huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano katika jengo la ofisi yake.
Ameueleza Mkutano huo kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwasaidia wananchi kwa nyanja mbalimbali hivyo ni lazima na watendaji waliochini yake wafuate utaratibu huo.
"Nawaagiza watembeleeni wafanyabiashara Ili msikilize changamoto zao na kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuwasaidia na msikae ofisini tu kusubiri mkutane nazo kwenye vikao kama hivi," amesema na akaongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, nishati na huduma za maji ambavyo vyote vinalenga kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Abdalah Ndauka alimuomba mkuu huyo wa Mkoa kuweka utaratibu utakaowezesha taasisi binafsi kushirikishwa kwenye vikao mbalimbali ili ziweze kutoa mchango wao wa mawazo yenye nia ya kujenga uchumi.
"Mhe. Mkuu wa Mkoa, nnaomba nikupongeze kwa juhudi zako za kutatua changamoto kwa wananchi, tangu umekuja hapa tumeanza kuona mabadiliko kadha wa kadha na mambo yanakwenda vizuri, lakini kwa baadhi ya watumishi wako bado hawaweki ushirikiano na sekta binafsi," alisema Ndauka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.